Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu bunifu zahitajika kukabili tatizo la ukosefu wa maji- FAO

Mwanamke kutoka  wilaya ya Dorkha , Nepal akitoka kuchota maji .
Piacha ya UNICEF/Narendra Shrestha
Mwanamke kutoka wilaya ya Dorkha , Nepal akitoka kuchota maji .

Mbinu bunifu zahitajika kukabili tatizo la ukosefu wa maji- FAO

Tabianchi na mazingira

Mkurugenzi Mkuu wa shrika la chakula na kilimo duniani, FAO José Graziano da Silva ametaka kuwepo kwa mbinu bunifu zaidi ili kuweza kukabiliana na tatizo la uhaba wa maji kwa nchi za kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Karibu, NENA.

Akizungumza kwenye mkutano unaojadili masuala ya maji na ardhi kwenye eneo hilo la NENA unaokunja jamvi hii leo huko Cairo, Misri, Bwana da Silva amesema ingawa hali mbaya za tabianchi pamoja na mizozo vimechochea ongezeko la njaa kwenye ukanda huo, bado uhaba wa maji nao unaweka watu  kwenye hali mbaya, hasa wale wa vijijijni wakilazimika kuhama makazi yao na kukimbilia mijni.

Amesema nchi moja kati ya tatu kwenye eneo hilo inatambuliwa kuwa ni maskini na sababu kuu ni ukosefu wa huduma ya maji akisema kuwa sekta ya kilimo ndio inawarudisha zaidi nyuma kutokana na ukosefu wa huduma hiyo.

 “Kuongeza ubunifu, sera na uwekezaji kwenye sekta ya maji kwenye ukanda huu wa Afrika ya Kaskazini na MAshariki ya Karibu ni jambo la msingi ili kuhakikisha maji hayakwamishi dira yetu ya kutokomeza aina zote za utapiamlo, kujenga amani ya endelevu na kutomwacha nyuma mtu yeyote,” amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO.

Sera ni zipi?

Akifafanua kuhusu sera hizo bunifu, Bwana da Silva amesema sera hizo za kizazi kipya lazima ziwe mtambuka zikileta pamoja seta za maji, chakula na biashara pamoja na kuweka mifumo ambamo kwayo wakulima wanaotumia maji na udongo kwa njia endelevu wanapatiwa motisha.

Bwana da Silva amesema, "ni lazima ikumbukwe kuwa ukosefu wa amji si lazima usababishwe na watu kukosa vyanzo vya maji kwenye eneo lao, bali maeneo mengi yanakosa maji kutokana na ukosefu wa uwekezaji.”

Ametaja sera bunifu kuwa ni pamoja na zile zinazochochea matumizi kidogo ya maji katika uzalishaji wa chakula, kilimo cha mazao yanayostahimili ukame, ufugaji wa mifugo isiyohitaji maji mengi, uvunaji wa maji na kuondoa chumvi kwenye maji ili yafae kwa matumizi ya binadamu na kilimo.

Amezipongeza nchi kama vile Algeria, Morocco, Jordan na Tunisia akisema zimechukua hatua muafaka kwenye kuvuna maji, Misri na Lebanon zikiwa na kasi kubwa ya umwagiliaji kwa njia yam atone pamoja na wengine wakichukua hatua kusafisha majitaka ili yatumike tena na tena,

Uhaba wa Maji na Utipwatipwa

Bwana da Silva pia kwenye hotuba yake amegusia uhusiano kati ya ukosefu wa maji na utipwatipwa akisema kutokana na jamii kukosa maji, eneo hilo linategemea zaidi vyakula vinavyoagizwa kutoka nchi za nje. “Hii inaweza kusababisha ongezeko la watu kuwa na uzito mkubwa na utipwatipwa. Soko la chakula duniani limerahisisha upatikanaji wa vyakula vya bei rahisi ambavyo hata hivyo vina kiwango kikubwa cha mafuta, sukari, chumvi.

Amesema mlo utokanao na vyakula vinavyopatikana kwenye eneo husika ni aghali kuliko vile vilivyoagizwa kutoka nje ambavyo viko kwenye makopo, “na hapa kwenye eneo la NENA takribani asilimia 30 ya watu wazima ni tipwatipwa kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani, WHO.”

Wakulima kama kitovu cha jawabu

Akitambua kuwa wakulima na kaya za vijijini ndio kitovu cha mkakati wa kukabiliana na uhaba wa maji, Bwana da Silva amesema “siyo tu kuwahamasisha kuanza kutumia teknolojia fanisi zaidi, bali pia kuwa na uwezo wa kupata maji safi na salama kwa ajili ya kaya zao. Hii ni muhimu sana kwa ajili ya uhakika wa kupata chakula na kuboresha lishe,”