Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame watishia maisha ya watu bilioni 2.5

Wakimbizi wa ndani wakimbilia Mogadishu Somalia wakitafuta msaada wa chakula na maji kufuatia ukame uliokithiri vijijini nchini humo.
Picha: OCHA
Wakimbizi wa ndani wakimbilia Mogadishu Somalia wakitafuta msaada wa chakula na maji kufuatia ukame uliokithiri vijijini nchini humo.

Ukame watishia maisha ya watu bilioni 2.5

Tabianchi na mazingira

Ukame umesababisha hasara ya dola bilioni 29 kwa mataifa yanayoendelea na tegemezi kwa kilimo katika kipindi cha miaka 11 iliyopita, imesema ripoti ya shirika la chakula na kilimo duniani FAO iliyotolewa leo huko Hanoi, Vietnam.

Ripoti hiyo imezinduliwa leo huko Hanoi, Vietnam na imeonyesha kuwa katika bara la Afrika, Amerika ya Kusini  na visiwa vya Karibea ukame ndio balaa kubwa kwa kusababisha hasara ya mimea ya dola milioni 10.7 ilhali mifugo ni dola bilioni13.

Hasara hiyo yote   ilitokea kati ya mwaka wa 2005 na 2015, imesema ripti ya FAO.

Ripoti ikionyesha kuwa watu takriban bilioni 2 na nusu duniani hutegemea kilimo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva amesema kuwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, hukumbana na vizingiti vingi.

Ametaja vizingiti hivyo kuwa ni pamoja na hali ya hewa, soko lisilotegemewa, wadudu waharibifu,magonjwa na migogoro isiyoisha.

Kwa ujumla ukame pamoja na majanga mengine ikiwemo mafuriko, matetemeko ya ardhi, mmomonyoko wa udongo, vimbunga na moto yamesababisha jumla ya hasara dola bilioni 96.

Bara la Asia limepata hasara ya dola bilioni 48 kutokana na majanga hayo yote.