Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tushikamane tujenge mustakhbali bora wa demokrasia – Guterres

Matembezi ya amani na demokrasia nchini Madagascar. Matembezi hayo yaliandaliwa na wanawake.
Photo: UNDP Madagascar
Matembezi ya amani na demokrasia nchini Madagascar. Matembezi hayo yaliandaliwa na wanawake.

Tushikamane tujenge mustakhbali bora wa demokrasia – Guterres

Masuala ya UM

Leo ni siku ya kimataifa ya demokrasia ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hakuna wakati ambao demokrasia imekuwa mashakani zaidi hivi sasa kuliko miongo kadhaa iliyopita.

Katika ujumbe wake wa siku hii amesema demokrasia inamaanisha kushughulikia usawa wa kisiasa na kiuchumi na kufanya demokrasia iwe jumuishi zaidi na kuwajumuisha vijana na walioenguliwa kwenye mfumo wa kisiasa.

Ni  kwa mantiki hiyo Bwana Guterres anataka siku hii itumiwe kusaka mbinu za kuchochea demokrasia na majibu ya changamoto za kimfumo zinazokabili dunia kwa sasa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa kujenga mustakhbali usioacha nyuma mtu yeyote kunahitaji kujibu maswali kadhaa.

Maswali hayo ni pamoja na je uhamiaji na mabadiliko ya tabianchi vitakuwa na athari gani kwa demokrasia kwa kizazi kijacho. Halikadhalika ni kwa jinsi gani dunia inaweza kutumia vyema teknolojia zinazobuniwa ili kuepusha hatari.

Na swali lingine alilotaka kila mtu ajiulize ni kwa vipi utawala bora unaweza kuimarisha demokrasia yenye maisha bora na kukidhi maslahi ya wananchi wote.

Katibu Mkuu amehitimisha ujumbe wake kwa kumtaka kila mtu kwa siku ya leo aazimie kuungana na wengine kujenga mustakhbali bora wa demokrasia.