Siku ya UN, Guterres asema changamoto ni nyingi "lakini katu hatukati tamaa"

24 Oktoba 2018

Leo ni siku ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni maadhimisho yanayolenga kusherehekea kuanza kutumika kwa katiba ya chombo hicho tarehe 24 Oktoba mwaka 1945.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake amesema “siku ya umoja wa mataifa huashiria kuzaliwa kwa mkataba wetu – nyaraka ya kipekee inayotoa matumaini, ndoto na matarajio ya “Sisi watu” akisema kwamba “kila siku, wanawake na wanaume wanaofanya kazi Umoja wa Mataifa hufanya kazi kwa vitendo kutekeleza mkataba huo.”

Katibu Mkuu amesema licha ya vikwazo, “hatukati tamaa. Umaskini uliokithiri unazidi kupungua, lakini tunaona ongezeko la kutokuwepo na usawa. Bado hatukati tamaa kwa sababu tunajua kwa kupunguza hali ya kutokuwa na usawa, tunaongeza imani na fursa za amani duniani kote.”

Ameongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanazidi kusonga kwa kasi kuliko wakazi wa dunia, “lakini hatukati tamaa kwa sababu tunafahamu kwamba hatua za kulinda tabianchi ndio njia pekee.”

UNDP Moldova
Nchini Moldova miradi ya Umoja wa Mataifa chini ya shirika lake la mpango wa maendeleo, UNDP na ubia na Muungano wa Ulaya, EU umeleta nafuu kwa kusaidiawafugaji wa nyuki kupata mazao bora

Kama hiyo haitoshi Bwana Guterres amesema “haki za binadamu zinakiukwa katika maeneo mengi. Lakini hatukati tamaa kwa sababu tunafahamu kuheshimu haki za binadamu na utu wa binadamu ni msingi wa amani.”

Ameangazia pia migogoro ambayo amesema inazidi kuongezeka, watu wanateseka.

Hata  hivyo Umoja wa Mataifa haukati tamaa “kwa sababu tunafahamu kuwa kila mwanaume, mwanamke na mtoto anastahili maisha yenye amani. Katika siku ya Umoja wa Mataifa, tuhakikishe tunaazimia upya ahadi yetu.”

Amesema ahadi hiyo ni kurekebisha uaminifu uliovunjika, kuiponya sayari ya dunia, kutomuacha nyuma mtu yeyote na kuzingatia utu wa kila mtu, kama Umoja wa Mataifa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud