Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi wa UN wana jukumu muhimu la kuhudumu, tuwalinde-Antonio Guterres.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres
UN /Manuel Elias
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres

Wafanyakazi wa UN wana jukumu muhimu la kuhudumu, tuwalinde-Antonio Guterres.

Masuala ya UM

Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alioutoa leo katika siku ya kimataifa ya kushikamana na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanaoshikiliwa au wasiofahamika walioko umeonesha kusikitishwa kwake na hali hiyo.

Ujumbe huo umemnukuu Bwana Guterres akisema, “usiku na mchana, kazi kwa kazi, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanafanya kazi pasi na kuchoka kuwasaidia watu walioko hatarini, kuilinda dunia na kujenga mstakabali bora kwa wote. Cha kusikitisha ni kuwa kutimiza wito huu, mara nyingi uhusisha hatari kubwa.”

Ujumbe huo umeendelea kueleza kuwa mwaka uliopita yaani 2018, wafanyakazai 16 wa Umoja wa Mataifa walitekwa, na kwa mwaka huu wa 2019 amepotea mfanyakazi mmoja. Katibu Mkuu ameshukuru kwamba wote hao wameachiwa lakini akaeleza kuwa kuna  wafanyakazi 21 wa Umoja wa Mataifa ambao wamekamatwa au kuwekwa kiuzuizini ambapo watano kati yao wanashikiliwa pasipo mashitaka yoyote.

"Tutaendelea kufanya kila lililo katika uwezo wetu kuwakomboa wenzetu” imesema taarifa hiyo

Aidha Bwana Guterres amesema katika siku hii ya kimataifa ya mshikamano na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walioko kizuizini au waliopotea, anatoa wito kwa nchi duniani kote kuunga mkono mkataba waliojiwekea mwaka 1994 kuhusu usalama wa wafanyakazi wa wa Umoja wa Mataifa na washirika wake. Hadi kufikia leo ni ni nchi 95 ambazo ni sehemu ya makubaliano hayo.

“Wawe katika nchi zao au nje ya nchi, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wana wajibu muhimu wa kuhudumia. Usalama wao unatakiwa kuwa kipaumbele chetu. Katika siku hii ya kimataifa, ninatoa wito kwa nchi zote wanachama na jumuiya ya kimataifa kuimarisha makubaliano ya kuwapa ulinzi wanaouhitaji na kuendelea na kazi yao ya amani na ustawi kwa wote” amesema Bwana Guterres.

Siku ya kimataifa ya mshikamano na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walioko kizuizini au waliopotea, inaadhimishwa kila mwaka katika kumbukumbu ya kutekwa kwa Alec Collett, mwanahabari wa zamani aliyekuwa akifanya kazi na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Palestina UNRWA na mtu mwenye silaha mnamo mwaka 1985. Hatimaye mwili wake ulipatikana katika bonde la Bekaa nchini Lebanon mwaka 2009.