Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wavenezuela wazidi kumiminika Colombia, WFP yasaidia

Raia wa Venezuela wanakwenda hadi Tumbes nchini Peru
Juliana Quintero na Inés Calderón / IOM
Raia wa Venezuela wanakwenda hadi Tumbes nchini Peru

Wavenezuela wazidi kumiminika Colombia, WFP yasaidia

Wahamiaji na Wakimbizi

Colombia inaendelea kukabiliwa na janga wakati huu ambapo maelfu ya raia wa Venezuela wanaendelea kumiminika nchini humo kila siku kutokana na uhaba wa chakula, dawa na mahitaji mengine muhimu nchini mwao.

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP linasema hadi sasa serikali ya Colombia na wanachi wake wanahaha kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuzingatia kuwa nchi hiyo imefanikiwa baada ya makubaliano ya amani na pia inahaha kutokomeza njaa lakini ujio wa wakimbizi wa Venezuela unarudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana.

Msemaji wa WFP huko Geneva, USwisi Herve Verhoosel amewaambia waandishi wa  habari hii leo kuwa ujio  huo unaathiri familia za wenyeji ambazo zinawapatia hifadhi kwa kuwa nazo zenyewe zinaishi mazingira magumu.

“Ni lazima tusaidie watu walionasa kwenye kile kinachotambuliwa kuwa janga la kikanda. Wahamiaji wanazidi kutumia njia ya Colombia kuingia Ecuador, Peru na mataifa mengine ya Amerika ya Kusini.na sasa serikali zimezidiwa uwezo,” amesema Bwana Verhoosel.

Kwa mantiki hiyo amesema hivi sasa WFP inaelekeza msaada wa chakula kwa wananchi wengi walio na shida huko Colombia na pia Ecuador ambako wahamiaji wengi kutoka Venezuela wanaelekea. Wengi wao wanaosaidiwa kwa mujibu wa Verhoosel ni wanawake na watoto ambao hawana huduma muhimu halikadhalika hawafahamu ni wapi watapata mlo wa siku inayofuata.

Amesema familia ya wahamiaji inapowasili kwenye makazi ya muda inapatiwa mlo wa moto na wanaweza kuishi eneo hilo kwa kati ya siku 3 hadi 5 na kwamba wanatakiwa kuondoka ili kutoa nafasi kwa wahamiaji wapya.

“Wengi wao wanakuwa hawana makazi na wanaishi kiholela na zaidi ya yote hawawezi kupata kazi na iwapo watapata mlo nao unakuwa si wenye lishe,” amesema msemaji  huyo wa WFP akisihi wahisani wasaidie kuchangia ili kuepusha zahma zaidi.

Tayari serikali ya Colombia imeomba msaada Umoja wa Mataifa kusaidia wimbi hilo la wakimbizi kutoka Colombia ambapo WFP imeazimia kuwasaidia kwa kuchangia mpango wa pamoja wa usaidizi kushughulikia suala la elimu, usalama, afya na lishe kwa wahamiaji hao.

TAGS: Colombia, Venezuela, WFP