Colombia yahitaji msaada kusaidia wakimbizi kutoka Venezuela

13 Machi 2018

Simulizi za watoto wa kike kulazimika kutumbukia kwenye biashara ya ngono ili waweze kujikimu maisha au watoto wa kiume kulazimika kuingia kwenye magenge haramu zimeshamiri miongoni mwa raia wa Venezuela wanaokimbilia Colombia.

Raia wa Venezuela wanaokimbilia Colombia kusaka mlo na huduma za tiba wamesimulia madhila wanayokumbana nayo ikiwemo uhaba wa huduma hata huko wanakokimbilia.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP David Beasley amenukuu simulizi hizo akizungumza na waandishi wa habari huko Bogota, Colombia akisema kuwa kutokana na shida huko Venezuela, raia kati ya elfu 40 na elfu 50 wanavuka mpaka kila siku na kuingia eneo la Cúcuta nchini Colombia.

Akinukuu baadhi ya simulizi hizo Bwana Beasley amesema..

(Sauti ya David Beasley)

“Mwanamke mmoja leo asubuhi amenisimulia jinsi ambayo mtoto wake wa kike anayeumwa vichomi, walikuwa hospitali ambako hakuna dawa wala chakula. Katika siku tano alizokuwa hospitali watoto 10 wamefariki dunia. Yeye aliamua kuondoka na mwanae ili waweze kuishi baada ya kubaini kuwa hawatapata msaada wowote.”

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa WFP amesema Colombia imepitia mambo mengi na sasa iko katika mwelekeo wa amani hivyo katu hawawezi kukubali janga hili la kibinadamu linalosababishwa na raia wa Venezuela kukimbilia nchini humo hivyo..

(Sauti ya David Beasley)

“Nimeahidi mbele ya rais kwa niaba ya shirika la mpango wa chakula duniani kuwa tutashirikiana kuandaa mpango wa kina wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia janga la kibinadamu Colombia na tutafanya kila tuwezalo ili kuondoa mzigo kwa raia wa Colombia.”

Serikali ya Venezuela hairuhusu Umoja wa Mataifa kuingia nchini humo ili kutathmini hali halisi au kutoa usaidizi.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter