Colombia inakabiliwa na janga kubwa:WFP

24 Septemba 2018

Colombia inakabiliwa na zahma kubwa wakati huu ambapo maelfu ya raia wa Venezuela wanaendelea kumiminika nchini humo kutokana na ukosefu wa chakula na mahitani mengine ya msingi nchini mwao.

Shirika la mpango wa chakula duniani,  WFP limesema hayo katika taarifa yake ya leo ikisema kuwa wimbi hili la uhamiaji kutoka Venezuela ni kubwa katika historia ya Amerika ya Kusini na limekuwa janga kubwa na linategemewa kuendelea.

WFP inasema wahamiaji wanaendelea kuitumia Colombia kama ushoroba au njia ya kuingia Ecuador, Peru na nchi nyingine za Amerika ya Kusini hali inayozipa ugumu serikali wenyeji.

Takribani watu 900 kwa siku wanavuka kuingia Cucuta, Colombia, wakitokea Venezuela ambapo Cucuta ndilo eneo ambalo lina kiwango cha juu cha wasio na ajira katika Colombia.

Daria Silva na familia yake walitembea hadi Cali wakitokea Cucuta akisema wameondoka nyumbani miezi mitatu iliyopita na nyumbani wameacha wanafamilia wengine.

“Ni hatari kwasababu tulikuwa kabisa tunakufa kwa njaa. Kila kitu kilikuwa kigumu kwetu. Hakuna dawa, hakuna chakula, hakuna chochote. Kila kitu kinazidi kuwa vibaya, vibaya, vibaya…watoto wanakufa!” Daria anasema.

WFP inasema wacolombia na serikali yao wanafanya kila waliwezalo kupambana na changamoto hii wakati huu ambapo tayari imepiga hatua katika mchakato wa amani na kumaliza njaa, ingawa wakati janga hili likikua linaweka hatarini maendeleo yaliyokwisha kufikiwa hivi karibuni.

Arliani Perez ni mama mwenye umri wa miaka 20. Yeye pamoja na bintiye mwenye umri wa miaka miwili aitwaye Aranny walitembea kutoka St. Cristobal, Venezuela hadi Bogata Colombia.

 “Wavenezuela wote wanafikiria kuondoka ili kutafuta utulivu. Lakini tunajikuta katika maeneo mengine…katika dunia nyingine ambayo si yetu. Imekuwa vigumu sana kwetu.”

Mgogoro huu unaziathiri familia na jumuiya zinazopokea idadi kubwa ya wahamiaji, hasahasa jamii za wenyeji ambao wanawapokea wageni wapya lakini wanakabiliwa na hali mbaya ya maisha.

WFP inatoa msaada wa chakula kwa walioko hatarini zaidi nchini Colombia na Ecuador hususani wanawake na watoto ambao kuzifikia huduma za msingi, wanakabiliana na hatari ya kukosa usalama na hawajui ambako wataupata mlo wao unaofuata.

Mkurugenzi wa WFP nchini Colombia, Bi Debora Hines anasema, “Mamilioni ya watu wameikimbia Venezuela wakiingia Colombia na nchi nyingine hali inayoleta janga katika ukanda huo. Janga hili la binadamu lina sura nyingi na watu hawa wanahitaji msaada wa chakula, ambacho WFP inasaidia. Jumuiya ya kimataifa inabidi kuingilia kati na kuhakikisha kuwa serikali katika ukanda huu zinasaidiwa”

Tangu kuanza kwa operesheni, WFP imeidhinisha misaada ya dharura ya chakula kwa wahamiaji 60,000 kutoka Venezuela katika vitengo vya mpaka vya Arauca, La Guajira na Norte de Santander. WFP hivi karibuni imeanza kufanya kazi katika kitengo kilichoko Nariño mpakani na Ecuador.

Takribani watu elfu 25 wamefikiwa kupitia mpango wa WFP katika Arauca, La Guajira na Norte de Santander. Kila siku WFP kupitia mpango huu wanatoa chakula moto mara mbili kwa watu walioko hatarini zaidi hususani wanawake, watoto na wazee, pia watu wenye ulemavu. Idadi ya watu wanaohitaji msaada inategemewa kuongezeka.

 

Wakati ongezeko la wahamiaji kuingia Colombia likitegemewa kuongezeka, WFP inategemea jumuiya ya kimataifa itaendelea kuunga mkono huduma za dharura. WFP inahitaji kwa haraka zaidi ya dola milioni 22 ili kukidhi mahitaji ya chakula na lishe ya wahamiaji wanaofika kutoka Venezuela.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter