Mafunzo ya kubadili tabia yaleta pamoja wakristu na waislamu CAR

11 Septemba 2018

Huko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu, MINUSCA unaendesha mafunzo yenye lengo la kupunguza ghasia na kuleta maelewano baina ya jamii, CVR.

Mafunzo hayo yaliyoanza tangu mwezi Mei mwaka huu  yanalenga siyo tu wanajamii wa kawaida bali pia wapiganaji ambao hivi sasa wamejisalimisha na kuachana na tabia hiyo.

Washiriki pamoja na stadi za maisha wanapatiwa mafunzo kuhusu kuondokana na silaha, ustaarabu, uraia ambapo hadi sasa kati ya wanufaika 885, wanawake ni 194.

Mmoja wa wanufaika ni Djamil Aboubakar ambaye amesema mafunzo hayo ambayo pia yanawapatia stadi za kujikwamua kimaisha, yamesaidia kuleta karibu jamii za wakristu na waislamu ambazo zimekuwa na uhasimu mkubwa uliosababisha hata mapigano.

Bwana Aboubakr amekiri kuwa mafunzo hayo yakiwa na maudhui kuishi pamoja yametuwezesha kuelewa madhara ya umiliki silaha kiharamu, na hivyo kusaidia kupunguza ghasia na kuimarisha usalama.

Naye mkufunzi Victor Kemby amesema washiriki wameweza kuelewana na kutambua umuhimu wa kuishi pamoja katika nchi hiyo ambayo imegubikwa na mzozo wa wenyewe kwa wenyewe kwa miaka kadhaa sasa.

Bwana Kemby amesema wameazimia kuendeleza maadili  haya waliyojifunza katika jamii zao.

Naye Meya ya mji wa Bambari Abel Matchipata amepongeza mpango huo akisema unapatia suluhu tatizo kubwa la ukosefu wa elimu na kunufaisha siy out washiriki wa mafunzo hayo bali pia jamii wanamoishi.

MINUSCA inatekeleza mradi huo kwa ushirikiano na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter