Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio dhidi ya hospitali CAR ni ukatili usiostahiki:UN

Mjini Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, operesheni za kibinadamu zinatatizwa na barabara mbaya, uhalifu, uporaji na machafuko ya makundi ya wanamgambo wenye silaha
OCHA/Gemma Cortes
Mjini Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, operesheni za kibinadamu zinatatizwa na barabara mbaya, uhalifu, uporaji na machafuko ya makundi ya wanamgambo wenye silaha

Shambulio dhidi ya hospitali CAR ni ukatili usiostahiki:UN

Amani na Usalama

Mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR amelaani vikali shambulio dhidi ya hospitali nchini humo na kusema sio ubinadamu na haustahili na ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Kundi la watu wenye silaha waliingia katika hospitali ya kanda katikati ya mji wa Bambari Jumamosi , baada ya kutoa vitisho siku ya Alhamisi kwa wahudumu wa afya na wagonjwa lakini pia hapo mwezi Mei kupora katika mashirika tisa ya kibinadamu na tume ya kitaifa ya wakimbizi 

Najat Rochid mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini humo (OCHA) analishutumu moja kwa moja kundi hilo lenye silaha kuhusika na madhara yoyote ya kitabibu na hali mahtuti ya wagonjwa.


Amekumbusha kwamba kwa kuzingatia misingi ya utu na ubinadamu , huduma za afya zinastahili zinatolewa kwa wagonjwa na kwa watu wote, hivyo kitendo walichokifanya kushambulia hospitali ni cha kikatili na kisichostahili.

Kwa miaka mitano sasa vita vimelighubika taifa hilo huku ghasia zikishika kasi mwaka uliopita. Duru za awali zinasema tangu kutokea kwa shambulio hilo ndugu wamehamisha wagonjwa 30 waliokuwa wamelazwa na kuwakosesha huduma za afya.

Bi. Rochdi amesisitiza kwamba hospitali za kiraia zinazotoa huduma kwa majeruhi na wagonjwa hazipaswi kushambuliwa kwa mazingira yoyote yale na hivyo kuasa kwamba ni lazima ziheshimiwe na kulindwa na pande zote katika mzozo.


Umoja a Mataifa unasema tukio hili linaongeza changamoto zaidi za kuchukua hatua za kibinadamu mjini Bambari hususan msaada wa kiafya.


Bi. Rochdi amesema “kwa mara nyingine raia wamekuwa mateka wa athari za mapigano baina ya makundi yenye silaha tangu Mei 14 na watu wamekoseshwa huduma za afya ambazo wanazihitaji sana.”
Hivyo “natoa wito kwa wahusika wa vitendo hivi vya kikatili, kuweka maslahi ya raia mbele badala ya tofauti zao.”