Ufisadi unapora mustakabali wa wananchi, taasisi na serikali zao:Guterres.

10 Septemba 2018

Kila nchi  na kila mdau katika jamii ana jukumu la kuhakikisha ufisadi unatokomezwa, kwani athari zake hazichagui wala hazibagui, ume masikini au tajiri, umeendelea au unajikongoja. Unapora haki za elimu, maendeleo, afya, uhuru na hata kuchochea migogoro

Onyo hilo limetolewa leo na Katibu Muu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani wakati wa kikao maalumu cha kujadili mbinu za kukabiliana na ufisadi ili kudumisha amani duniani.

Amesema ugonjwa wa ufisadi umetapakaa duniani nzima iwe ni kwa nchi masikini, tajiri, zilizoendelea na zinazoendelea n aza Kaskazini ama Kusini.Hivyo amessisitiza kwamba kupambana na ufisadi ni lazima wala sio chaguo kwani

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

“Unawapora watu wa haki zao, huwakimbiza uwekezaji wa kigeni na kuharibu mazingira. Ufisadi huchangia mapungufu ya serikali na utawala na mara nyingi husababisha kutowajibika kisiasa na kuvuruiga ushirikiano wa kijamii. Masikini na wasiojiweza wanateseka kwa kiasi kikubwa. Na ukwepaji sheria huzidisha ukubwa wa tatizo.”

Kwa upande wa masuala ya amani amesema

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES )

Ufisadi unaweza kuwa chanzo cha migogoro, na migogoro inaposhika kasi ufisadi unashamiri, na hata kama migogoro itasita, ufisadi unakuwa kikwazo cha kujikomboa upya. Ufisadi hushamiri kwa kusambaratisha taasisi za kisiasa na kijamii. Taasisi hizi hazijawahi kuwa katika msukosuko mkubwa kama wakati wa  mgogoro.”

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa kauli wakati wa mjadala kuadhimisha miaka 15 ya kuidhinisha mapatano ya Umoja wa Mataifa dhidi ya ufisadi.
UN/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa kauli wakati wa mjadala kuadhimisha miaka 15 ya kuidhinisha mapatano ya Umoja wa Mataifa dhidi ya ufisadi.

Ameongeza kuwa ufisadi pia unahisihwa na mambo mengi kama vile kutokuwa na utulivu na ghasia, usafirishaji haramu wa silaha, madawa ya kulevya nabinadamu.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu UNODC umebaini kwamba rushwa au hongo kwa maafisa wa umma iko katika kiwango cha juu hususan katika maeneo yaliyoathirika na migogoro.

Na ufisadi ukishika usukan , Guterres amesema athari zake ni mbaya sana hususan kwenye migogoro kwani zinaweza kuwanyima haki waathirika kupata huduma za msangi na kuongeza tatizo la njaa na umasikini. Hivyo ametoa wito

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES )

“Nchi wanachama ni lazima ziwe msitari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi. Ni muhimu hususan katika kujenga uwezo wa kitaifa wa tume za kupambana na ufisadi na juhudu za kuwaadhimisha. Nchi pia zinaweza kuimarisha juhudi za kupambana na ufisadi kwa kuhakikisha uhuru wa mahakama, asasi za kiraia , uhuru wa vyombo vya habari na ulinzi kwa watobia siri”

Kwa kutambua ukubwa wa tatizo la ufisadi barani Afrika , Muungano wa Afrika (AU) mwezi Januari mwaka huu ulizindua mwaka 2018 kuwa ni mwaka wa Afrika wa kupambana na ufisadi.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter