Skip to main content

Kilicho bora kwa Afrika ni bora kwetu sote- UN

Vijana wa Afrika wako mstari wa mbele katika ujasiriamali kama inavyoonekana pichanihuko Gambia walipotembelewa na mjumbe maalum wa UN kuhusu vijana, Jayathma Wickramanayake (kulia)
Alhagie Manka/ UNFPA Gambia
Vijana wa Afrika wako mstari wa mbele katika ujasiriamali kama inavyoonekana pichanihuko Gambia walipotembelewa na mjumbe maalum wa UN kuhusu vijana, Jayathma Wickramanayake (kulia)

Kilicho bora kwa Afrika ni bora kwetu sote- UN

Masuala ya UM

Miaka 55 iliyopita bara la Afrika lilizindua chombo chake kikileta pamoja nchi zilizokuwa zimepata uhuru. Hii leo  ni miaka 55!

Leo ni siku ya Afrika ikirejesha ulimwengu miaka 55 iliyopita ambapo ulizaliwa Umoja wa nchi huru za Afrika, OAU ambao sasa ni Muungano wa Afrika, AU.

Akizungumzia siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema kama ambavyo jina limebadilika, vivyo hivyo hali ya bara la Afrika.

Amesema hivi sasa kuna mafanikio makubwa akitaja uzinduzi wa hivi karibuni wa eneo la soko huru barani humo akisema litatochea ukuaji wa kiuchumi kwa wakazi bilioni 1.2 wa bara hilo na hatimaye kutokomeza umaskini.

Kama hiyo haitoshi amegusia kasi ya ukuaji wa ujasiriamali, idadi ya watoto wanaopata elimu pamoja na kupungua kwa vifo vya watoto wachanga huku wanawake wengi zaidi wakichaguliwa kuwakilisha jamii zao kwenye mabunge.

Watoto wanafunzi nchini Afrika Kusini
Benki ya Dunia/Trevor Samson
Watoto wanafunzi nchini Afrika Kusini

Bwana Guterres kwa sasa Afrika inazidi kuongeza kasi ya kujiendeleza kwa kuzingatia dira yake ya maendeleo yam waka 2063.

UN imedhamiria kuunga mkono juhudi za Afrika. Kwa mantiki hiyo taasisi hizi mbili mwaka jana zimetia saini makubaliano kuhusu mfumo wa amani na usalama pamoja na utekelezaji wa ajenda 2063 ya AU na ile ya UN ya 2030.

Amegusia pia suala la amani na maendeleo endelevu akifananisha na Ambari na Zinduna ya kwamba vinakwenda pamoja, hakuna kinachoweza kufanikiwa bila kujumuisha mwenzake.

Bwana Guterres amesema Umoja wa Mataifa utashirikiana na AU kusaidia mpango wake wa kuhakikisha mapigano barani humo yanasitishwa ifikapo mwaka 2020 huku akipaza sauti akisema, “katika siku hii ya Afrika, nasihi mataifa yote yaunge mkono azma ya Afrika yenye amani na ustawi. Kilicho bora kwa Afrika ni bora kwa dunia nzima.”