Wakimbizi Afrika Kusini wapaza kilio chao, UNHCR yasema imesikia na inachukua hatua

17 Oktoba 2019

Akihitimisha ziara yake ya siku mbili nchini Afrika Kusini, Kamishna Mkuu wa  shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi, ameelezea utayari wa shirika hilo kuendelea kusaidia serikali katika kuhakikisha ulinzi kwa wakimbizi na wasaka hifadhi nchini humo.

Ziara ya Bwana Grandi ilianzia kwenye  kituo cha usaidizi kwa wakimbizi na wasaka hifadhi kilichopo kwenye eneo la Hillbrow katika mji mkuu wa kibiashara wa Afrika Kusini, Johannesburg.

Wakimbizi na wasaka hifadhi wake kwa waume wameelezea madhila wanayopata ikiwemo kutothaminiwa na hata kutokuwa na nyaraka za kuwawezesha kupata matibabu.

Bwana Grandi akawaeleza kuwa amepokea maoni yao kwani lengo la ziara yake ni kujadili na serikali jinsi ya kupokea wasaka hifadhi na kuhakikisha wako salama na wanapata huduma za msingi.

Kisha alielekea mji mkuu Pretoria ambako amekuwa na mazungumzona Rais Cyril Ramaphosa na baadaye kusema kuwa “Afrika Kusini ina sera ya mfano ya kupokea watu wenye machungu kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika na kwingineko. Sasa bila shaka natambua ugumu. Tunashughulikia. Muwe na Subira na nafikiri chini ya uongozi wa serikali tutaweza kushughulikia baadhi ya masuala ambayo wakimbizi na wasaka hifadhi wameibua.”

Bwana Grandi pia alipata fursa ya kuzungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Jules yenye wanafunzi 900 wakiwemo wakimbizi, wasaka hifadhi na raia wa Afrika Kusini ambapo wanafunzi hao walionyesha uzoefu wao wa manufaa ya utangamano na Bwana Grandi akizungumza nao alisisitiza kuwa ukiwa mkimbizi hauko juu ya sheria.

Hata hivyo amewahakikishia kuwa, “kuna hofu kuhusu shinikizo kutoka kwa wageni, wahamiaji ambayo inahusisha pia wakimbizi. Rais amekuwa muwazi kuwa hii nchi haina stahamala kwenye vurugu. Taifa hili limetokana na harakati za kusaka  uhuru  dhidi ya ukosefu wa haki kwa hiyo ni lazima iheshimu maadili haya. Lakini pindi hali inapokuwa  ngumu kwa watu wengi wa taifa hili, ni vigumu zaidi kwa wakimbizi na wahamiaji kukubalika kwenye jamii na ndio maana tunashughulikia.”

Afrika Kusini inahifadhi wakimbizi na wasaka hifadhi zaidi ya 260,000 wengi wao wakitoka Somalia, Ethiopia, Zimbabwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Wakati wa ziara hii ya Grandi iliyofanyika takribani mwezi mmoja baada ya ghasia dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini zilizosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali nchini, Kamishna huyo pamoja na kuwa na mazungumzo na Rais Ramaphosa pia alikuwa na mazungumzo na wawakilishi wa mashirika ya kiraia, viongozi wa sekta binafsi, na viongozi waandamizi wa serikali.

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

UN yalaani ghasia dhidi ya wageni Afrika Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vitendo vya ghasia dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini vinavyoenda sambamba na mashumbulizi dhidi ya raia wa kigeni pamoja na uharibifu wa mali.