Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utesaji haukubaliki na haustahiki popote na kwa mazingira yoyote:UN

Utesaji
UNSMIL/Iason Athanasiadis
Utesaji

Utesaji haukubaliki na haustahiki popote na kwa mazingira yoyote:UN

Haki za binadamu

Utesaji unasalia kuwa ni kitendo kisichokubalika na kutohalalishwa wakati wowote ule na kwa sababu yoyote ikiwemo wakati wa hali ya dharura, vurugu za kisiasa au hata wakati wa vita

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo katika ujumbe wake kuhusu siku ya kimataifa ya mshikamano na msaada kwa waathirika wa utesaji, inayoadhimishwa kila mwaka Juni 26, akisisitiza kwamba ingawa hatua kubwa zimepiga katika kupunguza ukatili huo lakini bado juhudi zaidi zinahitajika ili kuukomesha kabisa.

Ametoa wito katika siku hii kuwaenzi na kushikamana na waathirika wa utesaji na familia zao na kuahidi kufanya kila liwezekanalo kukomesha utesaji.

Navyo vyombo vya Umoja wa Mataifa na vya kikanda vinavyopambana na utesaji, kwa kauli moja leo vimesema ahadi iliyoweka takribani miaka 70 iliyopita ya kuheshimu haki za binadamu ikiwemo kutotekeleza utesaji ambao ni kinyume cha sheria na utu, bado jinamizi hilo linaendelea katika maeneo yote duniani.

Vyombo hivyo ikiwemo ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa vimesema athari za utesaji ni kubwa sio tu kwa waathirika bali kwa jamii na hata vizazi na vizazi na zinaweza kuwa chachu ya kuleta mzunguko wa machafuko hasa waathirika wanaohisi hawathaminiwi. Zeid Ra’ad Al Hussein ni kamishina mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ansema

 

Image
Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’aad al-Hussein. UN/Jean-Marc Ferré

(SAUTI YA ZEID RA’AD AL HUSSEIN)

“Inachukua miongo kurejesha huyu muathirika katika hali ya kawaida kwa sababu ya mashambulizi ya kikatili katika mwili na akili yake, na ni dhahiri kwamba mfuko wa hiyari kwa ajili ya waathirika wa utesaji unajukumu muhimu sana. katika kila jamii kama walivyo waathirika wa ubaguzi na ukatili , ndio wanatakaoamua kuhusu utulivu katika jamii, wataamua endapo mikataba ya amani itadumu kwa muda mrefu, na kama hautawashughulikia na kuwasaidia , wataendelea kufungua vidonda katika jamii kwa sababu madhila yao hayajapata ufumbuzi”

Ameongeza kuwa tatizo lingine kubwa linalopaswa kushughulikiwa kimataifa ni ukwepaji sheria kwa wahusika wa utesaji kwani maelfu ya watu kote duniani ambao wamekuwa waathirika na wale ambao wanaendelea kuteswa hii leo hawapati haki zao kwa sababu watesaji  wanakwepa mkono wa sheria.