Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Magaidi waliua mpenzi wa maisha yangu na kuacha watoto bila mama-Manusura

Mohammed El Bachiri, muathirika wa ugaidi ambaye mke wake aliuawa kwenye shambulio la kigaidi huko Ubelgiji mwaka 2016.
UN /Mark Garten
Mohammed El Bachiri, muathirika wa ugaidi ambaye mke wake aliuawa kwenye shambulio la kigaidi huko Ubelgiji mwaka 2016.

Magaidi waliua mpenzi wa maisha yangu na kuacha watoto bila mama-Manusura

Amani na Usalama

Katika tukio la kuadhmisha kumbukizi ya kwanza ya waathirika wa vitendo vya ugaidi duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema sasa ni wakati wa kusikiliza wahanga hao akisema kuwa kusikiliza sauti zao na kuongeza msaada kwao na familia zao ni jambo jema kimaadili.
 

Akizungumza wakati wa tukio hilo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, lililoenda sambamba na kuzindua maonyesho ya kidijitali ya picha, video na simulizi za wahanga wa ugaidi, Guterres amesema “ugaidi ni changamoto kubwa zaidi ya zama za sasa.”

Maonyesho hayo yamepatiwa jina la “Kuendelea kuishi baada ya ugaidi: Sauti za manusura.”

Bwana Guterres amesema ni tishio kubwa la amani na usalama duniani na kwamba hakuna nchi ambaye inaweza kusema ni salama dhidi ya ugaidi.

Amesema manusura wa ugaidi ni kundi ambalo lina sauti muhimu zilizopo duniani ana ambazo zinaweza kutumika kukabiliana na ugaidi.

“Ni mara chache sana simulizi zao zinasikiliwa. Sasa ni wakati wa kupaza sauti zao na kutambua madhara ya ugaidi kwa maisha ya manusura hawa na familia zao, na wakati huo huo kuendelea kuwapatia msaada kwa njia bora zaidi,” amesema Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres, (wa pili kushoto) akimsalimia mmoja wa manusura wa ugaidi wakati wa kumbukizi ya kwanza ya waathirika wa ugaidi.
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres, (wa pili kushoto) akimsalimia mmoja wa manusura wa ugaidi wakati wa kumbukizi ya kwanza ya waathirika wa ugaidi.

Tukio hilo lilienda sambamba na kusikia ushuhuda kutoka kwa wahanga wa ugaidi na familia zao.

Miongoni mwao ni Mohamed El Bachiri, raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Morocco ambaye alipoteza mke wake kwenye shambulio la kigaidi lililotokea katika kituo cha treni ya chini ya ardhi huko Brussels, Ubelgiji mwaka 2016.

“Shambulio hilo lilichukua mpenzi wa maisha yangu na kuacha watoto wetu watatu bila mama,” amesema El Bachiri na kuongeza kuwa “shambulio hili ilikuwa ni kazi ya kikatili ya wahalifu waliojaa chuki ambao walijaribu kusaka kuhalalisha vitendo vyao viovu kwa kisingizio cha Mungu. Mungu wa chuki, uharibifu, uendawazimu, tofauti kabisa na Mungu wa upnedo, huruma na mwenye kufirikia, ambaye mimi binafsi naamini, na ambaye idadi kubwa ya waumini wa dini ya kiislamu wanaamini.”

El Bachiri ametoa wito kwa viongozi kuridhia sera ya huruma, nia njema na heshima kwa maisha ya binadamu na kwa raia wote bila kujali mipaka ya kisiasa na kijiografia.

Maonyesho hayo yanalenga kuonyesha gharama ya ugaidi kwa watu wa kawaida na jinsi kila manusura wa ugaidi anavyopata ujasiri wa kusimama na kutekeleza jukumu lake dhidi ya ugaidi na yataendelea hadi tarehe 4 mwezi ujao wa Septemba.