Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujasiri wa wafanyakazi wa UN wawezesha bendera yetu kupepea juu zaidi- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza hii leo katika tukio maalum kwenye makao makuu New York, la kuweka shada la maua kukumbuka waliopoteza maisha miaka 15 iliyopita kwenye shambulio huko Baghdad, Iraq
UN/Eskinder Debebe

Msaada wa Kibinadamu

Bendera ya buluu ya Umoja wa  Mataifa inapepea juu kabisa kwa sababu ya ujasiri wa wanawake na wanaume ambao wanaipeperusha mbali zaidi hadi kona mbali zaidi duniani.

Ni kauli ya Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, wakati wa kumbukizi ya miaka 15 tangu shambulio la bomu kwenye ofisi kuu za Umoja wa Mataifa huko Baghdad nchini Iraq.

Kumbukizi hiyo imefanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani ikiwa ni siku mbili kabla ya tarehe 19, ambapo ndio tukio lilitokea kwenye hotel ya Canal huko Baghdad, Iraq.

Katibu Mkuu amesema tukio hilo lilileta machungu sana kwa Umoja wa  Mataifa, ndugu na jamaa za marafiki za wafanyakazi 22 wa chombo hicho ambao walijitolea kwa ujasiri wao kwenda eneo hatarishi kuhudumia walio na  uhitaji zaidi.

Elipida Rouka, Afisa mwandamizi wa masuala ya siasa kwenye ofisi ya mjumbe maalum wa UN kuhusu Syria. Ni mmoja wa manusura wa shambulio la kwenye hoteli ya ya Canal, Baghdad tarehe 19 Agosti 2003. Hapa anaonyesha hati yake ya kusafiria ya UN iliyoharibiwa
UN /Violaine Martin

“Hili, kama alivyosema mkuu wa Baraza la Wafanyakazi,  lilikuwa ni shambulio kubwa la kwanza dhidi ya Umoja wa Mataifa. Lilileta majonzi kwa shirika zima, na tulijifunza mambo mazito. Mfumo uliokuwepo kwa ajili ya kufidia familia za wahanga ulikuwa hautoshelezi na imechukua muda mrefu kuiboresha,” amesema Katibu Mkuu.

Bendera ya buluu ya Umoja wa  Mataifa inapepea juu kabisa kwa sababu ya ujasiri wa wanawake na wanaume ambao wanaipeperusha hadi kona za mbali zaidi duniani.

Bwana Guterres amesema hata baada ya hapo watumishi wa  Umoja wa Mataifa wameendelea kulengwa kwenye mashambulizi na watu ambao wanataka kudhoofika kazi za Umoja wa Mataifa. “Kuanzia Algiers hadi Kabul, Mogadishu, Abuja na kwingineko na kwa lengo la kutunyamazisha na kututokomeza.”

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema ameazimia kuendelea kuimarisha usalama kwa watumishi wote wa Umoja wa Mataifa lakini akisisitiza kuwa kazi yao itaendelea kukumbwa na hatari.

Ingawa hivyo amesema mchangao wa wafanyakazi wa kujitolea, walinda amani, askari na watendaji wa kiraia ambao walijitolea uhai wao utaendelea kudumu kwenye nyoyo za watendaji wa shirika hilo.

“Njia pekee ya kuwaenzi ni kuendeleza kazi yao; kwenda kwenye maeneo hatari kwa lengo la kuwaweka salama wale walio na machungu na wanaotegemea misaada,” amehitimisha Katibu Mkuu.