Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu bunifu kuboresha ukusanyaji wa takwimu muhimu Afrika-UNICEF

Takwimu za wakimbizi na wahamiaji ni muhimu. Picha: UNHCR

Mbinu bunifu kuboresha ukusanyaji wa takwimu muhimu Afrika-UNICEF

Afya

Ikiwa leo ni siku ya usajili wa takwimu muhimu ikiwemo vizazi, talaka na vifo barani Afrika, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limekaribisha azma ya serikali za Afrika ya kuwekeza katika mifumo bunifu ya usajili wa taarifa hizo.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo huko Dakar Senegal na Nairobi Kenya imesema ahadi hiyo ni muhimu kwa kuzingatia hivi sasa barani humo ni takribani mtoto mmoja tu kati ya wawili mwenye umri wa miaka mitano ndio anayesajiliwa.

UNICEF inasema kwa mwelekeo huu watoto milioni 115 hawatakuwa na fursa ya utambulisho rasmi na hivyo kukosa huduma muhimu kwenye nchi yao ifikapo m waka 2030.

“Kimataifa, bara la Afrika ndio la chini zaidi katika usajili wa takwimu hizo muhimu na mfumo wake wa takwimu ni dhaifu,” amesema Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Leila Pakkala.

Bi. Pakkala amesema usajili baada ya kuzaliwa ni nyaraka muhimu ya ulinzi wa mtoto na pia kumwezesha kupata huduma za msingi.

 

Mama akiwa na watoto sita aomba msada .Je watoto hao wamesajiliwa? UNICEF yasema wazazi wazingatie kuwasajili watoto wao.
UNICEF
Mama akiwa na watoto sita aomba msada .Je watoto hao wamesajiliwa? UNICEF yasema wazazi wazingatie kuwasajili watoto wao.

 

Hata hivyo UNICEF imeweka matumaini katika teknolojia za kisasa ikisema ni fursa muhimu ya kuimarisha siyo tu usajili wa vizazi bali pia kujenga mifumo ya muda mrefu na ya kudumu ya usajili na ufuatiliaji.

Tayari UNICEF imeanzisha mbinu za kisasa na rahisi ambapo usajili wa vizazi na vifo unafanyika kwa njia ya simu ya kiganjani.

Mfumo huo wa usajili wa watoto unaojumuishwa na mifumo ya afya umezaa matunda nchini Uganda ambako kiwango cha usajili wa watoto wachanga kimeongezeka maradufu na kufikia asilimia 60.

Halikadhalika shirika hilo lina mkakati mwingine wa kushirikiana na mifumo ya afya na huduma ili kuhakikisha kila mtoto anahesabiwa na kupatiwa utambulisho kisheria.

Hii ni mara ya kwanza kwa bara la Afrika kuadhimisha siku hii ya takwimu muhimu kwa lengo la kuhakikisha kila mkazi anatambulika na hivyo kutoachwa nyuma katika ajenda 2063 ya bara hilo.