Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yaanzisha kampeni ya uhamasishaji umma kusaidia kudhibiti Ebola DRC

Dawa dhidi ya Ebola nchini DRC likipakuliwa kutoka kwa ndege Mavivi katika Kivu Kaskazini August 2018
MONUSCO-AVIATION
Dawa dhidi ya Ebola nchini DRC likipakuliwa kutoka kwa ndege Mavivi katika Kivu Kaskazini August 2018

UNICEF yaanzisha kampeni ya uhamasishaji umma kusaidia kudhibiti Ebola DRC

Afya

Wakati chanjo dhidi ya Ebola ikiendelea kutolewa huko jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nalo limepeleka wataalamu wake wa mawasiliano kwenye maeneo yaliyoathirika ili kuhamasisha jamii kuhusu chanjo hiyo.

Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC Dkt.Gianfranco Rotigliano amesema hayo leo kupitia taarifa iliyotolewa kwenye mji mkuu Kinshasa akisema mabingwa hao wa mawasiliano wamepelekwa majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.

Amesema wataalamu hao wanatoa ushauri nasaha kwa watu wanaopaswa kupata chanjo na pia kutoa taarifa muafaka kuhusu chanjo hiyo.

Dkt. Rotigliano, amesema sababu ya kupeleka wataalamu hao ni kutokana na kwamba katika mlipuko uliopita uhamasishaji wa jamii ulikuwa mbinu muhimu ya kuzuia kusambaa kwa Ebola na pia kuhakikisha watu wanashiriki katika kupata chanjo.

Timu ya WHO kwa msaada wa wakazi wa kijiji cha Bisolo, wakiweka magogo ili gari liweze kuvuka daraja na kuingia kijiji hicho kilicho umbali wa kilometa 25 kutoka kituo cha afya cya Iboko.
WHO
Timu ya WHO kwa msaada wa wakazi wa kijiji cha Bisolo, wakiweka magogo ili gari liweze kuvuka daraja na kuingia kijiji hicho kilicho umbali wa kilometa 25 kutoka kituo cha afya cya Iboko.

Kampeni hii ya kutoa chanjo ni ubia baina ya serikali ya DRC, UNICEF na shirika la afya ulimwenguni, WHO ambapo inatolewa bure na kwa hiari kwa mtu yeyote aliyekuwa na ukaribu na mtu aliyeugua au aliyefariki dunia.

UNICEF inasema kwa ushirikiano na wadau wake hadi sasa wameweza kufikisha ujumbe wa jinsi ya kujikinga dhidi ya Ebola  kwa viongozi wa jamii wapatao 60 katika maeneo yaliyoathirika ya Mangina  katika ukanda wa Mabalako.

Mbali na hayo pia wameweza kuwapatia mafunzo wafanyakazi 100 wa kijamii huko Beni ili nao waweze kutoa mafunzo kwa jamii zao.

Pia wameweza kusambaza ujumbe wa kinga dhidi ya ebola kwa makanisa 241 huko mjini Beni.