UN yalaani mauaji ya raia 200 yaliyofanywa na ISIL Syria
Umoja wa Mataifa umelaani shambulio la kutisha lililofanywa na magaidi wa ISIL kwenye maeneo yanayokaliwa na raia wengi huko jimbo la As-Sweida kusini-magharibi mwa Syria.
Msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani amesema hayo leo huko Geneva, Uswisi akizungumza nawaandishi habari akieleza kuwa wamepokea ripoti ya kwamba zaidi ya watu 200 waliuawa kwenye mashambulio lukuki.
Akifafanua zaidi kuhusu mashambulio hayo Bi. Shamdasani amesema, “wapiganaji kadhaa wa ISIL walivamia nyumba katika vijiji takriban vinane kwenye maeneo ya vijijini ya mashariki na kaskazini mwa As-Sweida mashambani, wakiwauwa raia kwa kuwapiga risasi ndani ya nyumba zao na kuwachukua mateka wanawake na watoto. Tumepokea majina 27 ya wanawake na watoto ambao wanaripotiwa kuchukuliwa mateka kutoka kijiji cha Al-Shbiki mashariki mwa As-Sweida vijijini, ingawa tunaamini idadi kamili inaweza kuwa kubwa zaidi ya hiyo.”
Amesema picha ya baadhi ya wanawake hao mateka baadaye zilichapishwa katika mtandao wa Twitter zikiambatana na vitisho kuwawatachomwa moto wakiwa hai iwapo serikali haitakomesha harakati zake za kijeshi dhidi ya wapiganaji wa ISIL katika maeneo ya magharibi mwa jimbo la Daraa na pia kuwaachilia huru wanawake na wanaume wa ISIL wanaoshkiliwa na serikali.
Bi. Shamdasan amesema wanaelewa kuwa wanamgambo wa ISIL wengi wao ni wale walioondolewa na kuhamishwa kutoka kambi ya wakimbizi wa kipalestina ya Yarmouk, Hajar Al-Aswadna Al-Tadamon kusini mwa Damascus kama sehemu ya mpango wa serikali wa makubaliano ya usuluhishi.
Imeripotiwa kuwa serikali inatumia makubaliano ya aina hiyo kwenye maeneo ambako inakaribia kuyatwaa ili kuyapatia makundi yaliyojihami uamuzi wa kuridhiana na serikali au kuhamishiwa maeneo ambako hayashikiliwa na serikali.
Amesema hatua ya kuhamisha wapiganaji inaweza kuleta hatari zaidi ya mashmbulizi kwa raia.
Kwa mantiki hiyo ameitaka serikali ya Syria kuwajibika kuchukua hatua kuzuia vitendo ambavyo vinaweza kuhatarisha maisha ya raia wa kawaida pamoja na kutoyaweka makundi yenye silaha kama vile ISIL katikati mwa raia.
Halikadhalika amesema serikali ya Syria ni lazima ihakikishe kuwa wale wote wanaotenda makosa ya jinai na wanaokiuka haki za binadamu wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria na viwango vya sheria za kimataifa.