Tuna hofu na kinachoendelea Saudi Arabia dhidi ya watetezi wa haki- UN
Umoja wa Mataifa una wasiwasi kutokana na visa vinavyoendelea nchini Saudi Arabia vya kuwakamata kiholela watetezi wa haki za binadamu pamoja na wanaharakati nchini humo ikiwemo wale wanaotetea haki za wanawake.
Wasiwasi huo umeelezwa na msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani akizungumza na waandishi habari leo mjini Geneva Uswisi.
Bi. Shamdasani amesema,“tangu tarehe 15 Mei, takriban watu 15 ambao wanaikosoa serikali wamekamatwa na tunaelewa kuwa wanane kati yao baadaye waliachiliwa huru kwa muda hadi kukamilishwa kwa kile kilichoitwa mapitio ya taratibu za kesi zao. Baadhi hawajulikani waliko na hakuna uwazi katika utaratibu wakushughulikia kesi zao.”
Ameongeza kuwa ingawa wahusika serikalini wametoa matangazo kuhusu uwezekano wa mashtaka makali dhidi yao , ambapo hukumu inaweza kuwa ya kuwafunga jela kwa kipindi cha miaka 20, bado haijaeleweka ikiwa mashtaka yamewekwa bayana katika kesi hizo zote.
Bi. Shamdasani ameihimiza serikali ya Saudi Arabia iwaachilie huru mara moja bila ya masharti yoyote wanaharakati wote na watetezi wa haki za binadamu ambao wamekamatwa kwa sababu za kazi zao ambazo wamekuwa wakifanya kwa njia za amani pamoja na kampeni ya muda mrefu iliyowezesha kuondolewa kwa marufuku ya wanawake kuendesha magari.
Msemaji huyo ameongeza kuwa uchunguzi wowote ule ni sharti ufanywe katika njia za wazi ambazo zinaheshimu haki zote na kwamba watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati wanapaswa kuenedelea na kazi zao muhimu za haki za binadamu bila hofu yoyote ya kushtakiwa.
Tags: Saudi Arabia,UN, Ravina Shamdasani,