Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Oparesheni ya kijeshi nchini Syria yasababisha maelfu kuhama, OHCHR yaingiwa na wasiwasi

Msichana wa umri wa miaka saba asimama mbele ya jengo la shule lililoharibiwa  mjini Idlib Syria.
UNISEF
Msichana wa umri wa miaka saba asimama mbele ya jengo la shule lililoharibiwa mjini Idlib Syria.

Oparesheni ya kijeshi nchini Syria yasababisha maelfu kuhama, OHCHR yaingiwa na wasiwasi

Haki za binadamu

Ofisi ya haki  za binadamu ya Umoja wa  Mataifa  OHCHR imeelezea wasiwasi wake kutokana na oparesheni  ya jeshi  katika mikoa ya Hama kaskazini na Idlib kusini nchini Syria iliyoanza  tangu Aprili 29, ambayo imeyaweka hatarini maisha ya maelfu ya watu waliokuwa wamehama makwao ambao wamekuwa wakiishi eneo hilo kwa miaka kadhaa.

Kwa mujibu wa msemaji wa ofisi hii mjini Geneva Uswis Ravina Shamdasani, wale wanaokimbia dhuluma wako katika hatari kubwa kwa usalama wao wanapokuwa safarini.

Ameongeza kuwa serikali na vikosi washirika wameongeza mashambulizi  kwenda maeneo ya vijijini huko Idlib kusini na Hama kaskazini. Sasa huenda oparesheni hiyo ya jeshi ikasababisha makundi mengi yenye silaha kujibu mashambulizi yakiwemo lile la Hay’at Tahrir al-Sham , kundi lenye uhusiano na lile la Al-Qaeda,  hatua ambayo itasababisha  kuwepo  ghasia zaidi.

Shamdasani amesema duru za kuaminika zinasema Kuongezaka  ghasia hizo tayari kumewaathiri sana raia. Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa  Mataifa, takriban raia 27 wameuawa na 31 kujeruhiwa tangu tarehe 29 Aprili wakiwemo wanawake wengi na watoto.

Maefu wamehana na wengi kuuawa

Mashambulizi kadhaa ya ardhini na ya angani yanaripotiwa kuendeshwa dhidi  ya miundo mbinu ya  raia kama vile shule na hospitali, hatua iliyosababisha uharibifu mkubwa.

Ofisi ya haki za binadamu inasema jana tarehe 6 Mei vikosi vya serikali vilianza kusonga mbele ambapo viliteka maeneo kutoka kwa  makundi yasiyounga mkono serikali huko Hama kaskazini.  Zaidi ya hayo makundi  yasiyo ya serikali yaliendesha mashambulizi huko Lattakia.

“Tarehe 30 Aprili raia watano waliuawa na 21 kujeruhiwa kwenye mashambulizi sita tofauti katika sehemu za  makaazi ya watu huko Idlib kusini na Hama kaskazini.  Moja ya mashambulizi hayo liligonga kituo cha afya huku lingine likipiga karibu na shule.”

Idlib nchini Syria kama ilivyo September 2018
WFP/Photolibrary
Idlib nchini Syria kama ilivyo September 2018

 

Oparesheni  hiyo ya jeshi  kadhalika imesababisha maelfu ya watu kuhama ambao  tayari washahama mara kadhaa na ambao  wamelazimika kueleka maeneo ya mbali kaskazini katika vijiji vya Idlib kaskazini na magharibi mwa Aleppo licha ya kuwa wako katika hatari ya kushambuliwa wakiwa njiani.

Ofisi ya haki za binadamu imetoa wito kwa pande zote katika mzozo kuheshimu misingi ya sheria za kimataifa za kibinadamu ya kutofautisha, kuchukua tahadhari na kuhakikisha raia na miundombinu yao wanalindwa.