UN yashikamana na Pakistan katika vita dhidi ya ugaidi -Guterres

25 Julai 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amelaani shambulio  la kujitoa mhanga lililotokea leo nchini Pakistan.

Shambulio hilo limetokea katika kituo kimoja cha kupigia kura mjini Queatta ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Baluchistan.

 Kwa mujibu wa duru za habari takriban watu 31 wameuawa wakiwemo polisi watano na watoto wawili na  wengine 35 wakijeruhiwa.

Shambulio limetokea leo wakati wananchi wa taifa hilo wakiwa kwenye uchaguzi mkuu kuamua nani ataliongoza taifa hilo kama waziri mkuu.

Shambulio hilo limefanyika  baada ya  mtu mmoja kujilipua alipokataliwa na polisi kuingia ndani ya kituo cha kupigia kura.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliothirika, watu na  serikali ya Pakistan.

Kupitia tarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Guterres amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unashikamana na kuunga mkono juhudi za serikali ya Pakistan katika vita vyake dhidi ya ugaidi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter