Huu ni ukatili na unachukiza-UNAMA.

22 Aprili 2018

Shambulio la kujitolea mhanga katika kituo cha kusajili wapiga kura  katika mji mkuu wa Afghanistan, na kusababisha vivyo vya takriban watu  30 na wengine 50 kujeruhiwa , limelaaniwa na mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Afghanistan, UNAMA.

Shambulio hilo lililotokea leo jumapili mjini Kabul ni la hivi karibuni kati ya mengine mengi yaliyotokea kwa nia ya kulenga  vituo vinavyohusiana na uchaguzi tangu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa wabunge na madiwani ambao umepangwa kufanyika  Oktoba 20 mwaka 2018. Mchakato wa kusajili wapiga kura ulianza wiki iliopita.

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Tadachi Yamamoto, amesema Umoja wa Mataifa unachukizwa na kukichukulia kitendo hicho kama  cha kikatili. 

Ameongeza kuwa bila kujali maisha ya wananchi,mauaji yaonekana kama sehemu isiyokubalika ya juhudi za wenye misimamo mikali  kuwazuia raia wa Afghanistan kutekeleza haki zao za kikatiba  za kushiriki katika uchaguzi.

Shambulio la leo limefanyika katika kituo cha kusajili wapiga kura kilichoko katika mtaa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ambapo mtu aliejitolea mhanga alijilipua akiwa katika kituo cha kugawa kadi za uchaguzi.

Siku ya Alhamisi, askari polisi wawili waliokuwa katika kituo cha kuwasajili wapiga kura mjini Jalalabad waliuawa kwa kupigwa risasi na watu waliokuwa na bunduki, na wiki iliyopita mjini Ghor, watu waliokuwa na silaha walichoma  kituo cha kuwasajili wapiga kura na kuwachukua mateka maafisa wa uchaguzi na wanausalama. Waliwaachilia siku iliyofuata, na Umoja wa Mataifa unataka waliofanya vitendo hivyo kuchukuliwa hatua za kinidhamu

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter