Tafadhali mnaovutana kuhusu Jammu na Kashmir msichukue hatua zitakazoathiri zaidi eneo hilo-Antonio Guterres.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, hii leo mjini New York Marekani, kupitia msemaji wake, ameeleza wasiwasi alionao kuhusu mgogogo unaoendelea katika eneo la Jammu na Kashmir, eneo linalovutaniwa kati ya India na Pakistani.
Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, “Katibu Mkuu amekuwa akiifuatilia hali ya Jammu na Kashmir kwa wasiwasi na amesihi kujizuia.”
Aidha kupitia taarifa hiyo Katibu Mkuu ameeleza kuwa msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhusu eneo hili unaongozwa na mkataba wa Umoja wa Mataifa na maazimio ya baraza la usalama.
Katibu Mkuu pia anarejelea makubaliano ya mwaka 1972 kuhusu uhusiano wa nchi mbili kati ya India na Pakistan, makubaliano ambayo pia yanafahamika kama makubaliano ya Simla, ambayo yanasema kuwa hatma ya mwisho ya hadhi ya Jammu na Kashmir yatafikiwa kwa njia za amani kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa.
“Katibu Mkuu pia ana wasiwasi na usambazaji zaidi wa vizuizi katika upande wa India wa Kashmir, hali ambayo inaweza kuzidisha hali mbaya dhidi ya haki za binadamu katika eneo hilo.” Imeeleza taarifa hiyo.
Vilevile Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande zote kutochukua hatua ambazo zinaweza kuathiri hali ya usalama ya Jammu na Kashmir.