Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu za kuigeuza Afrika kuwa na jamii endelevu na zenye mnepo kujadiliwa:UN

Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs  yako 17 na yanayopitiwa mwaka huu kwenye mkutano ulioanza leo ni malengo 6.
UN SDGs
Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yako 17 na yanayopitiwa mwaka huu kwenye mkutano ulioanza leo ni malengo 6.

Mbinu za kuigeuza Afrika kuwa na jamii endelevu na zenye mnepo kujadiliwa:UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Afrika endelevu na yeneye mnepo inawezekana umesema Umoja wa Mataifa hasa ikizingatia utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya bara hilo ya mwaka 2063 na ile ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030. Kinachohitajika ni mbinu mujarabu kufanikisha hilo.

Jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kufanyika kesho kesho Jumanne kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York Marekani ili kutathimini mbinu za kuibadili Afrika kuwa na jamii endelevu na zenye mnepo.

Jukwaa hilo la siku moja lililopewa kauli mbiu :Mabadiliko kuelekea jamii endelevu na zenye mnepo: kubaini mbinu za utekelezaji Afrika, lina lengo la kutanabaisha mbinu bora zitumikazo sasa, fursa na mapengo ya kielimu katika utekelezaji wa mikakati ya kusaidia mabadiliko ya kuelekea jamii endelevu na zenye mneno sanjari na ajenda ya maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063 na ile ya Umoja wa Mataifa ya 2030.

Jukwaa hilo litatoa fursa kwa washiriki kubadilishana mawazo ya matumizi bora ya mkakati wa utawala na nyenzo za kusaidia kuwa na jamii endelevu na zenye mnepo kwa muda mrefu.

Mkakati wa tathimini ya maendeleo Afrika na shirika kwa ajiliya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo OECD wamekuwa wakifanya kazi pamoja kubaini mbinu bunifu katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu au SDG’s.

Ubia ambao utazinduliwa katika jukwaa hili unatarajiwa kusaidia kuunda ushahidi wa ziada kote barani Afrika na pia kuainisha mbinu bora kutoka maeneo mengine.

Maelezo ya ziada

Wakati wa maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Muungano wa nchi za Afrika, wakuu wa nchi na serikali wa Muungano wa Afrika (AU) walipitisha uamuzi usio wa kawaida wa maono ya maendeleo ya muda mrefu yenye kichwa 'Afrika Tunayotaka'-Ajenda ya 2063 ambayo ililipa jukumu bara hilo la kuheshimu misingi ya demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria na utawala bora kwa kuchagiza usawa wa kijinsia, haki za kijamii kwa ajili ya maendeleo sawia, kuheshimu utu na maisha ya watu na kulaani mabadilo ya utawala yasiyo ya kikatiba.

Miaka miwili baadae jumuiya ya kimataifa ikapitisha ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030 na kuunda malengo 17 ya maendeleo ambayo yamekubatiwa na nchi na serikali zote za Afrika.

Hivyo ni muhimu sana kwa ajenda hizo mbili kutekelezwa kwa kuzingatia mikakati na vipaumbele vyake.

Nchi nyingi za Afrika zimechukua hatua za kuanzisha michakato ya mipango na kutekeleza malengo kama yalivyoainishwa kwenye ajenda ya 2063 na ile ya 2030 kwa ajili manufaa ya watu wao.