Dira 2020 ya kunyamazisha silaha Afrika yapatiwa ari mpya na azimio la UN

Watoto hawa zamani walikuwa wametumikishwa na vikundi vilivyojihami, hivi sasa wamejisalimisha na wako kwenye kambi ya Elevage huko Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR
UNICEF/Ashley Gilbertson
Watoto hawa zamani walikuwa wametumikishwa na vikundi vilivyojihami, hivi sasa wamejisalimisha na wako kwenye kambi ya Elevage huko Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR

Dira 2020 ya kunyamazisha silaha Afrika yapatiwa ari mpya na azimio la UN

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio lenye lengo la kufanikisha suala la kunyamazisha silaha barani Afrika, kwa kuzingatia kuwa mizozo inayorindima katika maeneo mbalimbali kwenye eneo hilo imekuwa kikwazo katika kufanikisha amani, usalama na maendeleo endelevu barani humo.

Azimio hilo limepitishwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani wakati wa mjadala wa wazi wa baraza hilo kuhusu kunyamazisha silaha barani Afrika.

Pamoja na mambo mengine, azimio hilo limekaribisha uamuzi wa Baraza la amani na usalama la Muungano wa Afrika, wa kutangaza kuwa kila mwezi Septemba ya kila mwaka hadi mwaka 2020 itakuwa ni mwezi wa kusalimisha silaha zilizomilikiwa kinyume cha sheria.

“Tunatambua kuwa kufanikisha unyamazishaji silaha Afrika kutachangia kwa kiasi kikubwa kuokoa vizazi na vizazi barani Afrika dhidi ya madhila ya vita, na pia tunatambua juhudi za Muungano wa Afrika kama zilivyobainishwa kwenye ajenda yake ya 2063 ya kuhakikisha zinajenga msingi wa amani na ustawi samamba na ajenda 2030 ya Umoja wa Mataifa,” limesema azimio hilo.

Mapema akihutubia baraza hilo, Mkuu wa Idara ya siara ya Umoja wa Mataifa Rosemary diCarlo amesema “Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika tuna msimamo  mmoja kuhusu nia yetu ya kuzuia mizozo. Kwa hiyo kunyamazisha silaha kunamaanisha pia kuzuia kwanza kabisa zisifyatuliwe..”

Vijana wa Bor jimboni Jonglei nchini Sudan Kusini wakivuna mazao kutoka kwenye shamba wanamopatiwa mafunzo na walida amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Korea Kusini
UNMISS
Vijana wa Bor jimboni Jonglei nchini Sudan Kusini wakivuna mazao kutoka kwenye shamba wanamopatiwa mafunzo na walida amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Korea Kusini

Amesema katika miaka miwili iliyopita, “tumeimarisha uwezo wetu wa pamoja wa kubaini na kutatua mizozo kabla haijaimarika sambamba na kushirikiana katika kusaidia kuitatu.”

Bi. DiCarlo ametaja baadhi ya mafanikio ya ushirikiano kati ya AU na UN kuwa ni pamoja na huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambako juhudi za pamoja kati yao zimefanikisha kutiwa saini kwa makubaliano ya amani kati ya serikali na waasi.

“Nchini Sudan Kusini nako mwaka jana kumetiwa saini mkabata mpya wa amani wenye nguvu mpya na umerejesha matumaini licha ya kwamba hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa”,  amesema Bi. diCarlo akiongeza kuwa ili hatimaye kunyamazisha silaha kwenye taifa hilo changa zaidi duniani.

Kupitia azimio hilo, wajumbe wa Baraza la Usalama wamemtaka Katibu Mkuu kwa mashauriano na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU wawe wanawapatia kwa wakati muafaka maendeleo ya utekelezaji wa hatua za kufanikisha usaidizi wa Umoja wa Mataifa na mashirika  yake kwa Muungano wa Afrika katika kukamilisha dira yake ya 2020 ya kunyamazisha silaha barani humo.