Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hebu na tuyaangazie mambo chanya barani Afrika- Kagame

Rais Paul Kagame wa Rwanda akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani tarehe 25 Septemba 2018
UN/Cia Pak
Rais Paul Kagame wa Rwanda akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani tarehe 25 Septemba 2018

Hebu na tuyaangazie mambo chanya barani Afrika- Kagame

Amani na Usalama

Rais Paul Kagame wa Rwanda amehutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kutaka kile alichokiita kuwa maendeleo chanya barani Afrika kisipuuzwe licha ya changamoto zinazokumba bara hilo.

Kagame ametolea mfano wa hatua za marekebisho ya muundo wa kifedha yaliyoanzishwa na Muungaon wa Afrika miaka mitatu iliyopita akisema yameanza kuzaa matunda.

“Tayari tunaona matunda. Nidhamu mpya ya matumizi ya fedha imewezesha bajeti ya Muungano wa Afrika, AU, kupungua kwa asilimia 12 ikilinganishwa na mwaka jana. Mchango wa fedha kutoka kwa nchi wanachama nao umekuwa bora kwa kuwa umeongezeka. Mchango katika fuko la amani ambao unasaidia AU kugharimia operesheni zake za ulinzi wa amani imefikia kiwango cha juu kabisa tangu kuanzishwa mwaka 1993.”

Na kama hiyo haitoshi, Rais Kagame ametolea  mkataba wa eneo  huru la biashara barani Afrika akisema kuwa kutiwa saini mwaka huu ni hitimisho la jitihada za miongo kadhaa.

“Pindi ikianza kufanya kazi, nafasi ya Afrika kwenye uchumi na muundo wa biashara duniani itapata ainisho jipya. Uokoaji wa gharama utokanao na faida ya kuongezeka kwa uzalishaji na viwango vya juu vya biashara baina ya nchi za Afrika vitasaidia barani letu kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, na pia uwezekano zaidi wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi kutokana na kukua kwa sekta binafsi Afrika.”

Amepongeza pia mabadiliko yanayotokea hivi sasa kwenye pembe ya Afrika ambako mahasimu wa siku nyingi, Eritrea na Ethiopia wameamua kuzika tofauti zao kwa maslahi  yao na wananchi wao.

Rais Kagame amesema ni jambo jema huku akiomba Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika washirikiane zaidi ili kusaka suluhu ya kudum ukwa mizozo huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Libya, ukanda wa Sahel na Sudan Kusini.