Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utandawazi wenye usawa ni mujarabu wa kusongesha SDGs Afrika- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na vyombo vya habari wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia
Daniel Getachew/UN Photo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na vyombo vya habari wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia

Utandawazi wenye usawa ni mujarabu wa kusongesha SDGs Afrika- Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Umoja wa Mataifa umesema kuwa bara la Afrika linahitaji utawandazi wenye usawa ili liweze kunufaika na mfumo wa biashara duniani.

 

Kauli hiyo imetolewa hii leo na Katibu Mkuu wa Umoja huo wa Mataifa Antonio Guterres wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Muungano wa Afrika, AU, mjini Addis Ababa, Ethiopia kunakofanyika mkutano wa mwaka wa viongozi wa chombo hicho chenye wanachama 54.

Guterres amesema hoja hiyo ilikuwa ni sehemu ya mazungumzo yake leo na viongozi wa Afrika hususan kuhusu kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs akisema kuwa katika suala hilo la utandawazi, “hapa napo tunataka kunufaika na mafanikio ya Afrika na maendeleo yake hasa katika eneo la biashara huru barani Afrika, AcFTA. Tunataka utandawazi wenye haki ili Afrika isikumbwa tena na machungu ya kanuni za biashara za kimataifa zisizo sawia, ruzuku na sera nyingine na masoko ambayo yanasongesha ukosefu wa usawa na hivyo kufanya bara la Afrika lishindwe kushindana na hata kustawi.”

 Eneo huru la biashara barani Afrika lilianzishwa tarehe 21 mwezi Machi mwaka 2018.

Mabadiliko ya tabianchi.

Bwana Guterres amesema pia wamejadili janga la mabadiliko ya tabianchi akisema kuwa“Afrika ina mchango mdogo sana katika janga hilo lakini ndio inaathirika zaidi. Ili kushughulikia hali hii, naendeleo kushinikiza usaidizi wa kimataifa kwa harakati za Afrika za kukabili na kuhimili madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwenye bara hili. Azma ya dunia inahitajika ili kufikisha ahadi ya kutokuwepo na utoaji wa hewa ya ukaa duniani ifikapo mwaka 2050, na hili la kutotoa hewa chafuzi linahusu pia wale wachafuzi wakuu.”

Katibu Mkuu ameweka bayana uhusiano kati ya baa la nzige nchini Ethiopia na maeneo ya nchi za Afrika Mashariki akisema kuwa, maji ya bahari yakiwa na joto ni mazingira bora zaidi kwa nzige kuzaliana. Hii leo uvamizi ufanywao na nzige ni mkubwa na hali inakuwa mbaya siku hadi siku. Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO linatueleza kuwa kundi la nzige sa na ukubwa wa mji mkuu wa Ufaransa, Paris linaweza kwa siku moja kumaliza chakula kinachokidhi mahitaji ya nusu ya wakazi wa Ufaransa.”

 Kwa mantiki hiyo ameelezea mshikamano wake na jamii zilizoathiriwa na baa la nzige akisema kuwa, “Umoa wa Mataifa umeshatangaza ombi la dharura la  usaidizi. Naomba jamii ya kimataifa iitikie wito huo wa usaidizi kwa kasi na ukarimu ili kuhakikisha kuwa tunachukua hatua sahihi za kudhibiti ongezeko la nzige hao wakati huu ambapo tuna fursa ya kufanya hivyo.”

Mshikamano wa AU na UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa mshikamano kati ya UN na AU ni muhimu san ana kwamba chombo hicho chenye wanachama 193, nchi za Afrika zikiwa ni miongoni mwao kinaunga mkono harakati za kusongesha amani, ustawi na haki za binadamu barani kote.

Amesema ushirikiano huo wa kimkakati kati ya vyombo hivyo viwili unazidi kuimarika siku hadi siku “kama mlivyoona asubuhi ya leo hususan mpango wetu wa kunyamazisha mtutu wa bunduki Afrika, haki za binadamu, usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu kwa mujibu wa ajenda 2030 ya Umoja wa Mataifa na ajenda 2063 ya AU.”

Amani Maziwa Makuu barani Afrika

Waandishi wa habari walitaka kufahamu msaada wa Umoja wa Mataifa katika juhudi za zinazoongozwa na Angola kama msuluhishi wa mzozo kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu ambapo Katibu Mkuu amesema kuwa, “nimekuwa nafuatilia kwa  karibu mkutano wa Luanda ulioleta pamoja viongozi wa Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na naunga mkono kwa dhati juhudi zao. Utulivu katika Maziwa Makuu ni muhimu kwa eneo zima la Afrika kwa kuzingatia uwepo wa eneo hilo na mahusiano yake na bara zima.”