Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chondechonde ruhusuni huduma za afya ziwafikie wahitaji kusini mwa Syria- WHO

Vituo vya kujihifadhi huko jimbo la Dara'a nchini SYria.
UNHCR/Bassam Diab
Vituo vya kujihifadhi huko jimbo la Dara'a nchini SYria.

Chondechonde ruhusuni huduma za afya ziwafikie wahitaji kusini mwa Syria- WHO

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la afya duniani, WHO limetoa wito kwa ulinzi wa vituo vya huduma za afya huko kusini mwa Syria sambamba na kutoa fursa zaidi kwa watoa misaada kuingia eneo hilo.

WHO imetoa wito huo kupitia taarifa yake iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi kwa kuzingatia kuwa hivi sasa mapigano yameshika kasi na watu zaidi ya 200,000 wamepoteza makazi yao na wana uhitaji mkubwa wa misaada ya dharura na huduma za matibabu.

Mathalani shirika hilo limesema watu wapatao 160 000 wamesaka hifadhi eneo la Quneitra ambako wahudumu wa afya hawawezi kufika na hivyo kuongeza wasiwasi kuhusu hali ya afya za wakimbizi hao.

Wiki iliyopita, takribani wasyria 15 wakiwemo watoto 12, wanawake 2 na mzee mmoja walifariki dunia kutokana na kukosa maji na magonjwa yatokanayo na kunywa maji machafu.

Mkurugenzi wa masuala ya dharura wa WHO kanda ya mashariki ya kati Dkt. Michel Thieren amesema wakazi wa maenoe ya Dar’a na Quneitra kusini mwa Syria wanawasubiri kwa hamu wahudumu wa kibinadamu ili wawafikishie misaada na hivyo hawawezi kuwaangusha.

“Tunatoa wito kwa pande zote kufungua milango yao ili dawa na vifaa vingine vya matibabu viweze kuwafikia wakazi hao wa kusini mwa Syria, lakini pia wawezesha majeruhi kuondoka salama na kwenda kwenye hospitali ambazo zinaweza kuokoa maisha yao,” amesema Dkt. Thieren.

Yaelezwa kuwa idadi kubwa ya wakimbizi hao wa ndani nchini Syria wanakabiliwa na msimu wa kiangazi wenye joto kali  ambapo viwango vya joto vimefikia hadi nyuzi joto 45 katika kipimo cha selsisyasi huku pepo za jangwani zikivuruma, maji safi na salama  yakiwa haba, huduma za kujisafi adimu halikadhalika huduma za afya.

WHO inasema wiki iliyopita, takribani wasyria 15 wakiwemo watoto 12, wanawake 2 na mzee mmoja walifariki dunia kutokana na kukosa maji na magonjwa yatokanayo na kunywa maji machafu.

Familia iliyosambaratishwa kutokaan na ghasia huko Dara'a kusini mwa Syria.
UNICEF/Alaa Al-Faqir
Familia iliyosambaratishwa kutokaan na ghasia huko Dara'a kusini mwa Syria.

Takribani asilimia 75 ya hospitali za umma na vituo vya afya huko Dar’a na Quneitra vimefungwa au vinafanya kazi chini ya uwezo wake na hivyo kusababisha majeruhi pamoja na wajawazito kushindwa kupata huduma za afya.