Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya kaskazini mwa Syria

Tarehe 11 Oktoba 2019 huko nchini Syria, mwanamke na wanae akiwa ameketi chini ya lori wakati huu ambapo wakimbizi wanawasili Ras al-Ain huko Tal Tamer, wakikimbia ghasia mpya kaskazini-mashariki mwa Syria.
© UNICEF/Delil Souleiman
Tarehe 11 Oktoba 2019 huko nchini Syria, mwanamke na wanae akiwa ameketi chini ya lori wakati huu ambapo wakimbizi wanawasili Ras al-Ain huko Tal Tamer, wakikimbia ghasia mpya kaskazini-mashariki mwa Syria.

WHO ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya kaskazini mwa Syria

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la afya duniani kuptia taarifa yake iliyotolewa mjini Cairo Misri, limeonesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya afya ya binadamu kaskazini mwa Syria ambako watu takribani 200,000 wameyakimbia makazi yao kutokana na ongezeko la operesheni za kijeshi tangu Oktoba 9 na hivyo watu milioni 1.5 wako katika uhitaji mkubwa wa huduma za kiafya. 

WHO imeeleza kuwa hivi sasa watu wapatao milioni 1.5 wako katika uhitaji mkubwa wa huduma za kiafya na wengi wao waliothiriwa na ukatili wa hivi karibuni tayari wamepata msongo mkubwa wa akili na akili ikiwa ni  matokeo ya miaka ya migogoro na kufurushwa mara kwa mara.

WHO imesema, watu walioko katika mahitaji makubwa ya huduma za kiafya wanakabiliana na changamoto zinazohusiana na ukosekanaji wa usalama na ufikiaji mdogo wa huduma za kiafya.

Imeongeza kuwa tayari miundombinu ya huduma za kiafya kaskazini mwa Syria zimeathirika sana kutokana na hali ya kukosekana kwa usalama iliyotokea hivi karibuni.

Hospitali ya taifa ya Al-Ain mjini Ras hivi sasa haitoi huduma na hospital nyingine ya taifa na vituo viwili vya afya mjini Tel Abyad vyote havifanyi kazi.

Vituo vyote vya afya katika kambi vilivyokuwa vinawapokea waliofurushwa Ain Issa na Ras Al Ain pia vimefungwa na watu kuahamishwa kutokana na kuongezeka kwa uwezekano wa kushambuliwa.

Nayo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA imeeleza kuwa hali mbaya na watu waliofurushwa wanakadiriwa kufikia kati ya 150,000 hadi 160,000 na ripoti za wengine wanaohama zinazidi kumiminika.

Mzozo wa Syria: Raia hawahusiki na chuki zenu- Guterres

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea hofu yake kubwa kuhusu mashambulizi ya kijeshi  yanayoendelea huko Kaskazini-Mashariki mwa Syria, mashambulizi ambayo tayari yamesababisha madhara kwa raia na takrbiani raia 160,000 wamekimbia makazi yao.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu ameendelea kuhisi pande  kinzani zijizuie na zitambue kuwa operesheni za kijeshi zinapaswa kuheshimu sheria ya kimataifa ikiwemo Katiba  ya Umoja wa Mataifa na sheria ya kibinadamu ya kimataifa.

Katibu Mkuu ametoa wito wa sitisho la mashambulizi haya mara moja na kusihi pande zote kinzani zisake suluhu kwa njia ya amani.

“Nasisitiza kuwa raia hawahusiki kwneye chuki na wanapaswa kulindwa wakati wote. Vivyo hiyvo, miundombinu ya kiraia inapaswa kulindwa kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu. Natambua hatari wanazokabiliana nazo raia walio wakimbizi wa ndani. Nasisitiza tena misaada ya kibinadamu iweze kufikishwa bila kikwazo chochote ikiwemo muundo wa kuwezesha Umoja wa Mataifa na wadau wake kuvuka mipaka bila vikwazo kuingia kaskazini-mashariki mwa Syria,” amesema Katibu Mkuu.

Halikadhalika Bwana Guterres ameeleza hofu yake kuwa kile kinachoendelea hivi sasa kinaweza kusababisha kuachiliwa huru kinyume cha inavyotarajiwa kwa watu wanaotuhumiwa kuwa na uhusiano na kikundi cha kigaidi cha ISIL, akisema hali hiyo itakuwa na madhara makubwa.

Amerejelea azimio namba 2254 la mwaka 2015 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalosisitiza kuwa suluhu yoyote kwenye mzozo wa Syria lazima lizingatia uhuru, mamlaka na umoja wa Syria.