Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wezesheni misaada ya kibinadamu iingie Syria- OCHA

Vituo vya kujihifadhi huko jimbo la Dara'a nchini SYria.
UNHCR/Bassam Diab
Vituo vya kujihifadhi huko jimbo la Dara'a nchini SYria.

Wezesheni misaada ya kibinadamu iingie Syria- OCHA

Amani na Usalama

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo wamejulishwa kuwa hali  ya usalama na kibinadamu nchini Syria inazidi kudorora kutokana na mashambulizi yanayoendelea hivi sasa dhidi ya raia hususan kusini mwa nchi hiyo.

Mkuu wa operesheni kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, John Ging amesema kwenye maeneo ya raia makombora yanaendelea kuporomoshwa kutoka angani  ambapo hadi leo hii watu wapatao 50,000 wamekimbia makazi yao.

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mapigano hayo ni yaliyoko jimbo la Dara’a lililoko mpakani na Jordan.

Bwana Ging amenukuu shirika la mpango wa chakula duniani, WFP likisema kuwa iwapo mashambulizi ya sasa yataendelea, idadi hiyo ya watu waliokimbia makazi yao inaweza kuongezeka maradufu.

“Makumi ya raia wameuawa, ikiwemo watoto na wengi zaidi wamejeruhiwa. Mashambulizi yameharibu pia miundombinu ya kiraia. Mathalani kombora moja la jana limeharibu hospitail moja huko Al-Hirak ishindwe kutoa huduma,”amesema bwana Ging ambaye aliwasilisha hotuba hiyo kwa niaba ya mkuu wa OCHA, Mark Lowcock.

Kama hiyo haitoshi amesema leo asubuhi vyombo vya habari vimeripoti kuwa mashambulio ya anga yameendelea na kuharibu hospitali ya Naseeb huko Dara’a ambako imelazimika kufungwa huku kurugenzi ya elimu ya jimbo la Dara’a likitangaza kuahirishwa kwa madarasa na mitihani yote.

Watoto wakiteka maji huko Douma, mji ulioko kwenye eneo la Ghouta Mashariki, nje kidogo ya mji mkuu wa Syria, Damascus.
UNICEF/Bassam Khabieh
Watoto wakiteka maji huko Douma, mji ulioko kwenye eneo la Ghouta Mashariki, nje kidogo ya mji mkuu wa Syria, Damascus.

Amezungumzia pia suala la usambazaji wa misaada ya kibinadamu akisema kuwa kutokana na mapigano yanayoendelea, misafara ya Umoja wa Mataifa inayoingia nchini humo imeahirishwa. Magari yaliyosheheni misaada yalikuwa yaingie kutoka Jordan.

“Kwa kuzingatia hali hii, narejelea wito aliotoa Katibu Mkuu wiki iliyopita wa kutaka kusitishwa mara moja kwa mwendelezo wa mashambulizi. Natoa pia wito kwa wadau wote kuhakikisha misafara  hii ya misaada ambayo inahusisha magari kuvuka mipaka, inaendelea bila ukomo,” amesisitiza Bwana Ging.

Akizungumzia maeneo ya Kaskazini-magharibi mwa Syria, hususan eneo la Idlib, Bwana Ging amesema hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya, ikihusishwa na idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao mwaka jana akisema kuwa  “zaidi ya watu laki tano walipoteza makazi yao huko Idlib katika miezi sita iliyopita. Kuna hofu pia ya mashambulizi ya kijeshi.”

Mkurugenzi huyo wa operesheni wa OCHA amesihi Baraza la Usalama liangazie ni jinsi gani ya kufanikisha ufikishaji wa misaada akisema, “kwa watu wengi wa kusini na kaskazini-magharibi mwa Syria, shehena hizo zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ndio tegemeo lao.”

Naye mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura, amehutubia baraza hilo kwa njia ya video kutoka Geneva, akisema kuwa anasikitishwa na kinachoendelea Syria, akionya kuwa kama hali itaendelea kama sasa, kile kilichotokea Aleppo na Ghouta kinaweza kutokea huko jimbo la Dara’a.

Amesihi pande zote kinzani Syria kutumia njia zozote zilizopo kuzuia machungu zaidi kwa binadamu.