Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgao wa WFP waingia Rukban Syria kwa mara ya kwanza, Guterres apongeza

Watu maelf kadhaa wakiwa wanahitaji msaada, msururu wa magari kama huu wenye shehena  ya msaada wa lishe upo ingawa mara kwa mara huwa unashambuliwa.
WFP/Marwa Awad
Watu maelf kadhaa wakiwa wanahitaji msaada, msururu wa magari kama huu wenye shehena ya msaada wa lishe upo ingawa mara kwa mara huwa unashambuliwa.

Mgao wa WFP waingia Rukban Syria kwa mara ya kwanza, Guterres apongeza

Msaada wa Kibinadamu

Hatimaye msafara wa magari yenye shehena za misaada ya kibinadamu umewasili ndani ya Syria na hivyo kuwezesha kwa mara ya kwanza shirika la mpango wa chakula duniani, WFP kusambaza misaada hiyo ndani ya taifa hilo lililogubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2011.

Taarifa ya WFP iliyotolewa hii leo inasema kuwa misaada hiyo itasambazwa kwa siku kadhaa kwa zaidi ya watu 50,000 walioko kwenye kambi ya Rukban, ambayo ni makazi yasiyo rasmi mpakani mwa Syria na Jordan.

“Eneo hilo lina mazingira gumu kwa kuwa ni la jangwani na limezingirwa na miamba,” imesema taarifa ya WFP ikiongeza kuwa msafara huo wenye malori 43 ya umesheheni vyakula kama vile magunia ya ngano.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha kitendo cha msafara huo kufikia wahitaji 50,000 hii leo huko kambini Rukban nchini Syria.

“Ufikishaji wa misaada hiyo ukijumuisha Umoja wa Mataifa na chama cha hilal nyekundu cha Syria unaruhusu pia watoa huduma za misaada kutoa chanjo za dharura kwa watoto wapatao 10,000 na pia kufanya tathmini ya haraka ya mahitaji,” amesema Bwana Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo mjini New York, Marekani.

Amesema ingawa inatambulika kuwa kutoa huduma za misaada iliyohitajika muda mrefu ni jambo muhimu, bado uwezo wa kufikisha misaada hiyo kwenye eneo hilo la jangwani hautoshi.

Mgao wa chakula kwa familia huleta angalau matumaini kwa watoto kama ionekanavyo kwenye picha hii baada ya mtoto kupata mgao kutoka WFP
WFP/Abeer Etefa
Mgao wa chakula kwa familia huleta angalau matumaini kwa watoto kama ionekanavyo kwenye picha hii baada ya mtoto kupata mgao kutoka WFP

Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande husika kuhakikisha kuwa ufikishaji wa misaada unafanyika bila vikwazo vyovyote ili kuweza kuwafikia wasyria wote hata walio maeneo ya ndani zaidi nchini Syria.
 
Misaada ya kibinadamu kwa wakazi hao wa kambi hiyo ya Rukban imekuwa si ya mara kwa mara kutokana na ukosefu wa usalama.

Awali WFP na wadau wengine wa kibinadamu waliweza kufikia eneo hilo kwa njia ambazo ziliwagharimu fedha nyingi na mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa mwezi Januari mwaka huu ambapo msaada ulisambazwa kupitia Jordan.

Ni kwa kuzingatia hilo, WFP imesema inahitaji uwezo wa kufikia wahitaji hao kila inapohitaji kufanya hivyo ili kukidhi mahitaji ya wanawake, watoto na wanaume ambayo ni chakula, maji na mahitaji mengine muhimu.

Maeneo mengine ya Syria ambako WFP imeweza kusambaza misaada ikiwemo nchini humo ni Al-Lajat liliko jimboni Dara’a ambako watu 27,500 wamefikiwa kwa mara ya kwanza tangu mapigano yaibuke kusini mwa Syria.
 
Hata hivyo WFP imesema inahitaji kusambaza chakula kwa watu milioni 3 nchini Syria kila mwezi ambapo chakula hicho ni mchele, ngano, mafuta ya kupikia, kunde, sukari na chumvi na kila mgao unaweza kulisha familia ya watu watano kwa mwezi mmoja.
 
Ili kufanikisha hilo, WFP kupitia taarifa yake inasema “ni muhimu WFP ipate fursa salama ya kufikia walio na mahitaji. Tuna matumaini kuwa pande zote zitaelewa kuwa WFP na Umoja wa Mataifa haziegemei upande wowote na uheshimiwe. Hivi sasa tunafanya kazi kusaidia raia na kuokoa familia.”