Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma duni za afya ni kwa nchi tajiri na maskini- Ripoti

Mhudumu wa kujitolea wa afya akijaza chanjo ya pepopunda kwenye bomba la sindano tayari kwa kampeni huko kaunti ya Koch nchini Sudan Kusini. Huduma hizi bila umakini zinaweza kuleta madhara kwa wahudumiwa.
UNICEF
Mhudumu wa kujitolea wa afya akijaza chanjo ya pepopunda kwenye bomba la sindano tayari kwa kampeni huko kaunti ya Koch nchini Sudan Kusini. Huduma hizi bila umakini zinaweza kuleta madhara kwa wahudumiwa.

Huduma duni za afya ni kwa nchi tajiri na maskini- Ripoti

Afya

Huduma duni za afya zinakwamisha maendeleo ya kuboresha afya katika nchi  bila kujali vipato vyao, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa na wadau wake. 

Ikiwa ni ushirikiano wa  shirika la ushirikiano wa maendeleo na uchumi, OECD, shirika la afya ulimwenguni, WHO na Benki ya Dunia, ripoti inasema kwa sasa, uchunguzi usio sahihi, kupatiwa dawa zisizo sahihi, matibabu yasiyofaa au yasiyohitajika, vifaa duni vya kliniki au watoa huduma wasio na mafunzo na stadi za kutosha ni mambo yaliyoko kwenye nchi zote maskini na tajiri.

Hali ni mbaya zaidi katika nchi maskini na za kipato cha kati ambapo asilimia 10 ya wagonjwa wakiwa  hospitalini wanaweza kuambukizwa magonjwa ikilinganishwa na asilimia saba katika nchi za kipato cha juu.

Hii ni pamoja na maambukizi ya hospitali yanayoweza kuepukwa kwa usafi bora na kubadili  mazoea ya kudhibiti maambukizi na matumizi sahihi ya viuavijidudu.

Ikipatiwa jina Kutoa Huduma bora za Afya –suala la lazima katika utoji huduma kote ulimwenguni, ripoti pia inasisitiza kuwa ugonjwa unaohusishwa na huduma duni za afya hugharimu zaidi  familia na mifumo ya afya.

Mhudumu wa afya akimhudumia  mmoja ya watoto waathirika wa utapiamlo Kasai DRC
Picha ya UNICEF/UN064905/
Mhudumu wa afya akimhudumia mmoja ya watoto waathirika wa utapiamlo Kasai DRC

Aidha huduma ya afya ya uzazi katika nchi nane zenye kiwango cha juu cha vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ni duni, huku ni asilimia 28 ya wanawake ndio wanapata huduma wakati wa ujauzito.

Katika mataifa ya kipato cha juu ripoti imesema asilimia 15 ya matumizi ya hospitali ni katika kushughulikia maambukizi yatokanayo na makosa ya utunzaji mgonjwa akiwa hospitalini.

Hata hivyo ripoti inataja maendeleo fulani katika kuboresha ubora ikiwemo ongezeko la muda wa kuishi kwa wagonjwa wa saratani  na moyo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema shirika lake linajitolea kuhakikisha kuwa watu wote kila mahali wanaweza kupata huduma bora za afya wakati na mahali wanapohitaji  kwa kuwa bila huduma bora hakuna upatikanaji wa huduma za afya kwa wote.

TAGS: WHO, OECD, BENKI YA DUNIA, Tedros Adhanom Ghebreyesus, AFYA