Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kudhibiti hewa chafuzi ni gharama lakini kutoidhibiti ni gharama kubwa zaidi- WHO

Kiwango cha uchafuzi wa hewa ni cha juu kiasi kwamba mtoto huyu amelazimika kuvaa barakoa wakati akisubiri basi kwenye kituo kimoja huko Ulaanbaatar nchini Mongolia
UNICEF/Mungunkhishig Batbaatar
Kiwango cha uchafuzi wa hewa ni cha juu kiasi kwamba mtoto huyu amelazimika kuvaa barakoa wakati akisubiri basi kwenye kituo kimoja huko Ulaanbaatar nchini Mongolia

Kudhibiti hewa chafuzi ni gharama lakini kutoidhibiti ni gharama kubwa zaidi- WHO

Afya

Mkutano wa kwanza wa kimataifa kuhusu uchafuzi wa hewa na afya umeanza leo huko Geneva, Uswisi ambapo Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni Dkt. Tedros Ghebreyesus ametumia hotuba ya ufunguzi kuweka bayana takwimu za vifo na madhila yatokanayo na uvutaji wa hewa chafuzi.

Akifungua mkutano huo wa siku tatu utakaomalizika tarehe mosi mwezi ujao, amesema “hebu na niwakumbushe takwimu. Uchafuzi wa hewa unaua watu milioni 7 kila mwaka. Watu 9 kati ya 10 wanavuta hewa iliyochafuliwa na moshi wa kwenye magari, viwanda, shughuli za kilimo na hata moshi utokao kwenye mitambo ya kuteketeza taka.”

Tutashirikiana na watendaji katika sekta ya usafiri, mipango miji, makazi, nishati na mazingira kwa kuwapatia mbinu, rasilimali na kusaidia kutathmini madhara ya kiafya yatokanayo na maamuzi yao ya kisera.

Amesema makadirio ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa theluthi moja ya vifo vitokanavyo na shambulio la moyo, kiharusi, saratani ya mapafu na magonjwa sugu ya njia ya hali ya hewa yanasababishwa na hewa chafuzi akisema kuwa, “watu bilioni 3 wanaendelea kutumia majiko yasiyo rafiki kwa mazingira ambayo yanatoa moshi mzito, na baya zaidi majiko hayo yanatumika ndani ya nyumba.”

Mkuu huyo wa WHO ambayo ndiyo imeandaa mkutano amesema ingawa kuna hofu, bado kuna matumaini kwa kuwa vifo hivyo vya watu milioni 7 kila mwaka vinaweza kuepukika na hivyo kuna hatua ya kuchukua.. "itahitaji utashi thabiti wa kisiasa, hatua za haraka na azma ya dhati lakini nina nina matumaini kuwa tunaweza, ni lazima na tuchukue hatua bora zaidi. Ninakubaliana kuwa gharama ya kuchukua hatua ni kubwa lakini gharama ya kutochukua hatua ni kubwa zaidi.”

Ametaja hatua za kuchukua ili hewa inayovutwa iwe bora na salama kuwa ni pamoja na zile ambazo WHO imeshaanza kuchukua ambazo ni kuwezesha wataalamu wa afya kuelezea madhara ya hewa chafuzi kwa wagonjwa na jinsi ya kupunguza madhara hayo.

Kwenye miji kama Beijing nchini China, ukungu ni tatizo kubwa la kiafya.
WMO/Alfred Lee
Kwenye miji kama Beijing nchini China, ukungu ni tatizo kubwa la kiafya.

Amehitimisha hotuba  yake kwa kusema kuwa hakuna mtu, kundi, mji, nchi au eneo ambalo linaweza kutatua suala hilo la uchafuzi wa hewa pekee, badala yake amesisitiza ushirikiano wa kila pande, serikali, viongozi wa kijamii, mameya, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na mtu mmoja mmoja.