Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa FAO na EU ‘kupiga jeki’ familia zilizoko hatarini Iraq

Wakimbizi wa Iraq waliopoteza makazi kufuatia vita Mosul wanatengeneza chakula kambini Hamsansham, Iraq. Picha: UNHCR/Ivor Prickett

Mradi wa FAO na EU ‘kupiga jeki’ familia zilizoko hatarini Iraq

Msaada wa Kibinadamu

Jamii zilizoko hatarini katika maeneo yaliyokuwa na vita katika eneo la bonde la Ninewa magharibi mwa Mosul nchini Iraq zitaweza kuwa namnepo, kufuatia mradi wa Euro milioni 6 uliofadhiliwa na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO na Muungano wa Ulaya, EU.

Mradi huo ambao ni sehemu ya programu ya ukarabati na uwezeshaji wa FAO unalenga kuimarisha kipato cha kila kaya huku ikikarabati miundombinu na kuanzisha miradi inayozalisha kipato.

Mradi unalenga kaya 1,250 na utawezesha watu hususan wanawake na jamii zilizotengwa kupata kipato kwa kufanya kazi ambapo watu 7,500 watanufaika.

FAO imesema matokeo ya kazi hiyo ni kwamba yatawezesha wakulima kupata maji kwa ajili ya umwagiliaji na mifugo yao kufuatia kukarabati kwa eneo la kuvuna maji, barabara, na mitaro.

FAO inahitaji dola milioni 10.2 kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji na wakulima 116,100 katika masuala ya mifugo, kukabiliana na wadudu wanaokula mimea na kuhakikisha uhakika wa chakula.

Aidha shirika hilo limesema linahitaji dola milioni 76 kwa ajili ya kusaidia watu milioni 1.6 katika kipindi kirefu kwa ajili ya kuwezesha jamii.

FAO inalenga kuhakikisha familia za vijijini zina rasilimali za kujenga upya maisha na kupata kipato kwa ajili ya mustakbali wao.

Kwa ushirikiano na serikali ya Iraq, FAO inalenga kuwezesha jamii kurejea maeneo yaliyonyakuliwa, wakimbizi wa ndani na wanaowahifadhi na wakimbizi kutoka Syria.