Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata wafungasha virago wahudumu wa afya Iraq

Raia katika mji wa Mosul, Iraq baada ya shambulio la gari la  kujitoa mhanga.
UNHCR/Ivor Prickett
Raia katika mji wa Mosul, Iraq baada ya shambulio la gari la kujitoa mhanga.

Ukata wafungasha virago wahudumu wa afya Iraq

Msaada wa Kibinadamu

Ukosefu wa fedha unatishia kufungwa kwa vituo muhimu vya afya nchini Iraq na hivyo kuacha mamilioni  ya watu bila fursa ya kupata dawa muhimu na huduma ya afya.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO kupitia taarifa  yake iliyotolewa mjini Baghdad, Iraq hii leo limesema usaidizi kwa huduma za afya Iraq  unapungua kwa kasi kubwa tangu kumalizika kwa kampeni ya kukomboa mji wa Mosul mwaka mmoja uliopita.

WHO inasema tayari wadau wanne wa shirika hilo wamefunga vituo 22 vya kutoa huduma muhimu za afya kwa mwaka huu wa 2018 kutokana na uhaba wa pesa na hivyo kuacha pengo kubwa  katika utoaji wa huduma za kiafya kwa watoto, wanawake na wanaume ambao bado hawana pa kwenda pamoja na wale waliorejea makwao huku miundombinu  ikiwa imesambaratishwa.

Taarifa inaongeza kuwa asilimia 38 ya vituo vya afya ambavyo vinasaidiwa na washirika wanane wa afya vinatishiwa kufungwa  ifikapo mwisho wa mwezi wa Julai, na hivyo kuongeza hatari ya  kutokea mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza na hilo kurudisha nyuma juhudi zilizokuwa zimefikiwa  katika maeneo yaliyoharibiwa wakati wa mapambano.

Pesa zinazohitajika kugharimia huduma  za mpango wa kusaidia masuala ya kibinadamu Iraq ni dola za kimarekani milioni 67.4. 

Hata hivyo WHO inasema mpaka sasa ni asilimia 12.5 iliyopatikana ambayo ni sawa na dola milioni 8.4.

WHO inasema kati ya fedha hizo zinazohitajika haraka na washirika wa afya chini ya mpango wa kibinadamu ni dola milioni 54 ili kutoa huduma kwenye majimbo ambayo yamenza kufikika tena hivi sasa.

Kwa sasa vituo hivi vinatoa huduma za kifya kwa watu zaidi ya  waIraqi 900,000 ambao hawana makazi  pamoja na wenyeji wao.