Ziara ya Papa Francis Iraq ni ishara ya matumaini- UNESCO

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis amewasili nchini Iraq hii leo kwa ziara ya siku tatu, ziara ambayo shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO inasema ni ishara ya matumaini na fursa ya kuimarisha jitihada za amani, na umoja nchini humo.
UNESCO kupitia taarifa yake imesisitiza “ziara ya Papa Francis inakuja na ujumbe wa amani na umoja ikiungwa mkono na utofauti wa wairaq. Ujumbe huu uko katika mamlaka yetu kuu ya kuelewana, kuheshimiana na hatimaye kuwa na dunia yenye amani na haki.”
Papa Francis aliwasili Iraq siku ya Ijumaa na anatarajiwa kuwasili kwenye mji wa kaskazini wa Mosul siku ya Jumapili, ambako vyombo vya habari vinasema atasali na waathirika wa mzozo unaosababishwa na magaidi wa ISIL ambao wamesababisha vifo vya maelfu ya watu.
Ziara ya Mosul inabeba ujumbe muhimu, imesema UNESCO, mji ambao ni wa kale zaidi duniani na kituo cha kitamaduni na kidini, mji ambao umekumbwa na uharibifu mkubwa tangu magaidi wa ISIL wadhibiti mji huo kati yam waka 2014 hadi 2017.
Katika kipindi hicho cha miaka mitatu, kumekuwepo na mapigano kadhaa, na kusababisha mji huo kubakia mahame, huku maeneo ya kihistoria yakisalia magofu yakiwemo majengo ya historia ya kidini, kitamaduni huku maelefu ya wakazi wa mji huo wakisalia wakimbizi na makovu makubwa na mahitaji makubwa ya kibinadamu.
Kufuatia kukombolewa kwa mji huo, UNESCO na wadau wake ikiwemo serikali ya Iraq, wamekuwa wakishirikiana kusongesha urithi wa kipekee wa kitamaduni na kidini pamoja na kutumia elimu kuondokana na misimamo mikali.
“Ni kupitia elimu na utamaduni ambao wanawake na wanaume wa Iraq wanao wataweza kupata tena udhibiti wa mustakabali wao na kuwa watekelezaji wa kurejesha upya nchi yao,” amesema Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO katika ujumbe wake.
The city of #Mosul is...🏛 one of the world’s oldest cities☮ cultural crossroad of coexistence🇮🇶 living symbol of Iraqi’s pluralistic identity@UNESCO's #ReviveTheSpiritOfMosul brings hope for the city and its people. https://t.co/YTpG7q0BZx #PopeFrancisinIraq pic.twitter.com/mxrgj6LOWh
UNESCO
Mpango wa kipekee wa UNESCO uitwao “Rejesha nafsi ya Mosul”, uliozinduliwa mwezi Februari mwaka 2018 ni picha kamili ya hatua ya shirika hilo la kurejesha upya mji wa Mosul katika hali yake.
Mpango huo unajikita katika siyo tu kujenga upya maeneo ya urithi wa dunia wa mji huo bali pia kuwawezesha wakazi wa mji huo kuwa mawakala wa mabadiliko wanaoshiriki katika ujenzi mpya wa mji wao kupitia utamaduni na elimu.
Kama hatua ya kwanza ya kukwamua Mosul, UNESCO inakarabati mnara wake mashuhuru uliopinda sambamba na makanisa ya Al-Tahera na Al-Saa’a. Shirika hilo pia limeanza ukarabati wa msikiti wa Al-Aghawat na nyumba za kale kwenye mji huo.
Pamoja na ukarabati wa majengo maarufu ambayo ni alama za mji huo, mpago pia unajumuisha mafunzo kazini kwa wataalamu vijana, kuimarisha uwezo wa wasanii wa kazi za sanaa za uchongaji, kuweka fursa za ajira na elimu ya kiufundi na ufundi stadi.