Kudhibiti kuenea kwa silaha, tuondoke maofisini twende mashinani

UNMAS iki katakata bunduki kwa ushirikiano na  tume ya kitaifa ya silaha ndogondogo ya Ivory Coast(COMNAT-CI)
Picha: UNOCI
UNMAS iki katakata bunduki kwa ushirikiano na tume ya kitaifa ya silaha ndogondogo ya Ivory Coast(COMNAT-CI)

Kudhibiti kuenea kwa silaha, tuondoke maofisini twende mashinani

Amani na Usalama

Mikakati mipya inahitajika ili kuweza kudhibiti kuenea kwa silaha ndogo na zile za kawaida ambazo kwa kiasi kikubwa ndio zinatumiwa kwenye migogoro duniani hivi sasa.

Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa katika kudhibiti kuenea kwa silaha Izumi Nakamitsu amesema hayo leo jijini New York, Marekani wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati huu ambapo kuna mkutano wa tatu wa mapitio kuhusu udhibiti wa silaha ndogo na za kawaida.

Bi. Nakamitsu amesema mikakati hiyo mipya ni pamoja na kupanua wigo wa wadau ambao wanafanya nao kazi badala ya kujikita na serikali pekee akisema ..

 (Sauti ya Izumi Nakamitsu)

 “Katika mazingira mengi hususan kwenye ujenzi wa amani itaamanisha kusaka mbinu mbadala za kujipatia kipato kwa wapiganaji wa zamani, itaamanisha pia kufanya kazi na serikali za mitaa, serikali za manispaa na kufanya kazi na mashirika ya mashinani na muhimu zaidi kushirikisha vijana.

 Bi. Nakamitsu akasema mikakati hiyo mipya ya kufika mashinani ni muhimu kwa kuwa itasaidia kuwapatia vijana na makundi mengine mbinu za kujipatia kipato na kuachana na matumizi ya silaha ndogo na za kawaida katika kuchochea mizozo na ghasia kwenye maeneo yao.

 “Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana Katibu Mkuu Guterres mwezi uliopita alizindua ajenda yake ya kudhibiti kuenea silaha ambapo moja ya misingi ya ajenda hiyo ni kuokoa Maisha,” amesema mwakilishi huyo wa ngazi ya juu.

 Mkutano huo wa wiki mbili ulioanza jana jumatatu, unapitia maendeleo ya utekelezaji wa mpango wa wa kuzuia, kukabili na kutokomeza biashara haramu ya silaha ndogo na nyepesi kwa kuzingatia kanuni za kimataifa za ufuatiliaji wa silaha hizo.