Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuitikie wito wa ‘Hibakusha’, tutokomeza silaha za nyuklia- Guterres

Wingu zito baada ya kuangushwa kwa bomu la atomiki kwenye mji wa Hiroshima. Picha hii ilipigwa saa 2.17 asubuhi ikiwa ni dakika mbili baada ya bomu kuangushwa.
UN /Mitsuo Matsushige
Wingu zito baada ya kuangushwa kwa bomu la atomiki kwenye mji wa Hiroshima. Picha hii ilipigwa saa 2.17 asubuhi ikiwa ni dakika mbili baada ya bomu kuangushwa.

Tuitikie wito wa ‘Hibakusha’, tutokomeza silaha za nyuklia- Guterres

Amani na Usalama

Hii leo dunia ikifanya kumbukizi ya miaka 74 tangu Marekani iangushe bomu la nyuklia kwenye mji wa Hiroshima nchini Japani, bado mvutano mkubwa kati ya mataifa yenye silaha za nyuklia unaendelea na kutia hatarini amani na usalama ulimwenguni.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake hii leo huko Hiroshima na msaidizi wake wa  masuala ya kudhibiti kuenea kwa silaha duniani, Izumi Nakamitsu.

Guterres amesema “ni heshima kubwa kukumbuka waliopoteza maisha wakati bomu hilo lilipoangushwa pamoja na wengine wengi ambao maisha yao yalisambaratishwa kutokana na madhara ya muda mrefu wa minururisho ya bomu hilo la nyuklia.”

Katibu Mkuu amesema hatua zilizochukuliwa baada ya shambulio hilo kubwa la tarehe 6 Agosti mwaka 1946 ni pamoja na kilio cha dunia nzima kuhakikisha kuwa silaha za nyuklia katu hazitotumika tena.

Mabaki ya moja ya majengo huko Hiroshima nchini Japan baada ya kuangushwa kwa bomu la atomiki Agosti 6, 2018
UN
Mabaki ya moja ya majengo huko Hiroshima nchini Japan baada ya kuangushwa kwa bomu la atomiki Agosti 6, 2018

“Wakazi wa Hiroshima na Nagasaki, wakiongozwa na manusura majasiri wa wa shambulio la Hiroshima na lile la Nagasaki wamekuwa mstari wa mbele. Dunia ina deni kubwa kwa ujasiri wao wa kuongoza kimaadili na kutukumbusha juu ya gharama anayobeba binadamu kutokana na vita vya nyuklia,” amesema Katibu Mkuu.

Hata hivyo amesema kuwa cha kusikitisha hali ya usalama iko hatarini kutokana na mivutano baina ya mataifa yanayomiliki silaha hizo, “nyezo na taasisi zinazodhibiti silaha hadi kufanya dunia kuwa pahala salama hivi sasa zimeibuliwa hoja.”

Bwana Guterres amesema ni vyema kila mtu akumbuke kuwa manusura hao wa hibakusha, wamesafiri ulimwenguni kote wakieneza  ujumbe kuwa hakikisho pekee dhidi ya matumizi ya silaha za nyuklia ni kutokomeza kabisa silaha hizo.

Amekumbusha kuwa kuzuia matumizi ya silaha za nyuklia, ilikuwa ndio azimio la kwanza kabisa la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1946. “Lengo hili ni msingi wa ajenda yetu mpya ya kudhibiti kuenea kwa silaha ambayo niliwasilisha mwaka jana. Leo hii, narejelea tena wito wangu kwa viongozi wa dunia kuongeza juhudi zao kuelekea lengo hilo,” amesema Guterres.

Tarehe 18 disemba 2015, Yasuaki Yamashita, mmoja wa manusura wa shambulio la Nagasaki wajulikanao kama Hibakusha kwa kijapan na ambaye sasa anaishi Mexico, alikuwa na mazungumzo na wafanyakazi wanatoa huduma za ziara ndani  ya UN, jijini New York, Marekan
UN/Jihye Shin
Tarehe 18 disemba 2015, Yasuaki Yamashita, mmoja wa manusura wa shambulio la Nagasaki wajulikanao kama Hibakusha kwa kijapan na ambaye sasa anaishi Mexico, alikuwa na mazungumzo na wafanyakazi wanatoa huduma za ziara ndani ya UN, jijini New York, Marekani

Katibu Mkuu ameweka takwimu bayana kuwa wakati huu wa miaka 74 tangu shambulio la Hiroshima,  takribani duniani hivi sasa kuna vichwa 1,400 vya nyuklia, ambavyo vingi vyao vinasubiri tu kufyatuliwa.

Ametamatisha hotuba yake akisema kuwa, “kazi kubwa imesalia kupunguza na hatimaye kuondokana na tatizo hili. Nikimasishwa na mnepo na moyo wa watu wa Hiroshima, nimeazimia kushirikiana na Hibakusha na wengine wote kufikia lengo letu la pamoja, dunia isiyo kuwa na silaha za nyuklia.”