Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkakati kuongeza rutuba na kuepuka mmomonyoko wa udongo Afrika

Udongo wenye rutuba huwezesha kupata mazao bora. (Picha@Unifeed)

Mkakati kuongeza rutuba na kuepuka mmomonyoko wa udongo Afrika

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO na mshirika wake wa kimataifa wa masuala ya udongo leo wamezindua mkakati mpya wa kuboresha rutba na kupunguza mmomonyoko wa udongo kwa ajili ya kuhakika wa chakula na lishe barani Afrika.

Mkakati huo uliopewa jina “Udongo wa Afrika” (Afrisoils) una lengo la kuongeza kiwango cha uzalishaji cha udongo kwa asilimia 30 katika mataifa 47 ya Afrika na kupunguza mmomonyoko wa udongo kwa asilimi 25 katika miaka 10 ijayo.

Kwa mujibu wa FAO Afrika ni bara la pili kwa kuwa kavu duniani huku karibu nusu ya eneo lake ni jangwa na asilimia 40 limeathirika na hali ya jangwa.

Pia takwimu zinazonyesha kwamba takribani asilimia 65 ya eneo la kilimo barani Afrika limeathirika na mmomonyoko wa udongo uliosababisha kupoteza rutba na vitutubisho muhimu kwa ajili ya uzalishaji wa chakula.

FAO inasema endapo udongo ukiathirika kiasi hicho inakuwa ni vigumu sana na gharama kubwa kuurejesha katika hali yake ya awali.

Licha ya jitihada za kuboresha kilimo barani Afrika , kwa jumla bara hilo linasalia kuwa na changamoto kubwa za uhakika wa chakula ambao unaathiri takriban asilimia 70 ya watu wake ambao wanategemea kilimo na kati ya watu milioni 815 walioathirika na lishe duni,  milioni 243 kati yao wako barani Afrika.