Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji wa teknolojia ya kidijitali ni muhimu katika kufanikisha SDGs-UNCTAD

Katibu Mkuu wa kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD Dkt. Mukhisa Kituyi
UN News/Grece Kaneiya
Katibu Mkuu wa kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD Dkt. Mukhisa Kituyi

Uwekezaji wa teknolojia ya kidijitali ni muhimu katika kufanikisha SDGs-UNCTAD

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Teknolojia ya kidijitali inatoa fursa za maendeleo ambazo ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa kuelekea ukomo wake mwaka 2030, lakini pia ina changamoto zake.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mtendaji wa Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi, awali katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa hapa jijini New York, Marekani. Hata hivyo Dkti. Kituyi amesema ni muhimu kwa kila taifa kuwekeza katika miundomsingi ya teknolojia za kidijitali, jambo ambalo amesema nchi za Afrika bado zinasua sua nalo.

(Sauti ya Kituyi)

"Mataifa mengi ya Afrika hayajafika kiwango hiki.  Lakini hata yale ambayo yamejitahidi, kama Afrika Kusini, Kenya, Nigeria, Morocco, yanagundua kuna changamoto nyingine kubwa sana. Kwamba raia wengi wanatumia dijitali kama  watumiaji, wale wanaotumia mtandao, michezo ya mtandao, facebook, lakini sio kama wenye wanabuni rasilmali, wanabuni faida. Kutengeneza huduma ya kuuza nyumbani au kwa mataifa ya kigeni kunahitaji kuwekeza katika talanta ya kutumia hii dijitali kama fursa. Kuwepo tu na broadbend haileti faida pekee yake."

Ameongeza kwamba faida za teknolojia hii inatoa fursa zaidi kwani

(Sauti ya Kituyi)

"Teknolojia ya kidijitali inaweza kusaidia kuona soko, ukatambua kwamba unataka kuuza kitu katika hilo soko lakini utahitaji barabara na reli na ndege, kufikisha bidhaa zako katika hilo soko.  Sasa angalau unawekeza katika broadbend unahitaji kuwekeza tena kwa mbinu za kusafirisha zile ambazo unajaribu kuuza. Sasa hayo yote yanalingana pamoja."