Tusipowekeza katika afya ya akili, msalaba wake kijamii na kiuchumi hautobebeka:WHO

6 Juni 2018

Ili kutimiza malengo ya afya kimataifa ni lazima kuwekeza katika afya ya akili na kuepusha mzigo mkubwa wa kijamii na kiuchumi limesema leo shirika la afya ulimwenguni WHO.

WHO imeainisha hayo katika kitabu kilichotolewa leo  kinachooenyesha mwenendo wa afya ya akili duniani mwaka 2017 na kudhihirisha kwamba ingawa kuna baadhi ya nchi zimepiga hatua katika kuweka mipango na sera kuhusu afya ya akili, bado kuna upungufu mkubwa kote duniani wa wahudumu wenye ujuzi wa afya ya akili na pia ukpungufu wa uwekezaji katika vituo vya kijamii vya afya ya akili.

Kwa mujibu wa Dr Shekhar Saxena , mkurugenzi wa idara ya afya ya akili na matumizi mabaya ya mdawa wa WHO , kitabu hiki kinatoa ushahidi kwamba kuongeza rasilimali katika afya ya akili hakufanyiki haraka kama inavyostahili.

Muuguzi akizungumza na wagonjwa wenye matatizo ya afya ya akili.(Picha:WHO/Marko Kokic)
Muuguzi akizungumza na wagonjwa wenye matatizo ya afya ya akili.(Picha:WHO/Marko Kokic)

 

Amesema kushindwa kuwekeza katika afya ya akili kama suala la dharura , kutakuwa na gharama kubwa za kiafa katika jamii na uchumi katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, na isitoshe itakuwa mtihani mkubwa kutimiza malengo ya maendeleo endelevu SDG’s hususan ya afya.

Kitabu hicho pia kimetoa taarifa ya sera zilizopo, mipango na sheria kwa ajili ya afya ya akili, na zinavyokwenda sanjari na kuanzisha nvyombo vya haki za binadamu , lakini pia rasiklimali za kifedha zilizopo kwa, aina za vituo vinavyotoa huduma, na program za kuzuia na kuchagiza masuala ya afya ya akili.

Kitabu hicho kimetokana na takwimu zilizotolewa na nchi 177 wanachama wa WHO, ambao ni asilimia 97 ya watu wote duniani na kinapima kiwango cha nchi kuimarisha uongozi na udhibiti wa afya ya akili. 

Kituo cha afya cha muda cha kutibu watu wenye matatizo ya afya ya akili.(Picha:UM/ WHO/A. Bhatiasevi)
Kituo cha afya cha muda cha kutibu watu wenye matatizo ya afya ya akili.(Picha:UM/ WHO/A. Bhatiasevi)

WHO inasema katika nchi za kipato cha nchini kiwango cha wahudumu wa afya ya akili kinaweza kuwa kidogo hadi kufikia wahudumu 2 kwa watu 100,000 ikilinganishwa na wahudumu zaidi ya 70 kwa nchi zilizoendelea. Na hii haiwiani na matarajio ya WHO kwamba kila mtu 1 kati ya 10 atahitaji huduma ya afya ya akili katika wakati fulani wa maisha yake.

Chini ya nusu ya nchi 139 zilizo na mipango na sera za afya ya akili, ndizo zilizojumuisha sera hizo sanjari na miakataba ya haki za binadamu ambayo inasisitiza umuhimu wa kujumuisha waathirika kutoka katika vituo vya afya aya akali na kuingia katika huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha katika maamuzi yanayowahusu.

TAGS: WHO, afya ya akili, SDG’s

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud