UN yasihi utulivu na maelewano Mali

2 Juni 2018

Huko Mali kuelekea uchaguzi wa rais mwezi ujao, polisi wa kutuliza ghasia wapambana na wafuasi wa vyama vya upinzani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametaka utulivu nchini Mali sambamba na pande kinzani zijizuie kuchukua hatua zitakazoweza kuleta madhara zaidi,  kufuatia mapigano kati ya waandamanaji na polisi wa kutuliza ghasia kwenye mji mkuu Bamako.

Yaelezwa kuwa ghasia hizo ziliibuka leo wakati polisi walipotumia mabomu ya kutoa machozi kujaribu kuzuia waunga mkono wa maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika mjini humo kudai uwazi zaidi wakati huu ambapo uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika mwezi ujao.

Katibu Mkuu kupitia msemaji wake amerejelea kile alichoshuhudia wiki hii  wakati wa ziara yake nchini Mali ambacho ni “maendeleo katika utekelezaji wa mkataba wa amani na maridhiano akisihi mwelekeo huo uendelee hadi kufanyika kwa uchaguzi.”

Bwana Guterres amesema anasikitishwa na kitendo kwamba serikali  ya Mali imezuia maandamano ya vyama vya upinzani, akisisitiza kuwa mazungumzo jumuishi ya kisiasa ni muhimu kama ilivyo kuzingatia haki za msingi ikiwemo ya kujieleza na kufanya maandamano ya amani.

Katibu Mkuu akiwa ziarani nchini Mali wiki hii kwa maadhimisho ya siku ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, alipata fursa ya kuzungumza na viongozi mbalimbali ikiwemo pande zilizotia saini mkataba wa amani na maridhiano miaka mitatu iliyopita.

Alisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa umeazimia kusaidia suluhu ya amani ya mzozo nchini Mali. 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter