Ulinzi wa amani ni uwekezaji wa amani- UN

29 Mei 2018

Leo ni siku ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, UN ikilenga kutambua mchango wa wanawake na wanaume zaidi ya milioni moja waliohudumu kama walinda amani wa chombo hicho tangu kuanzishwa kwa operesheni hizo miaka 70 iliyopita.

Katika kuadhimisha siku hii, Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres yuko nchini Mali ambako azma ni kuonyesha mshikamano na walinda amani walioko nchini humo katika moja ya operesheni hatari zaidi za ulinzi wa amani za chombo hicho MINUSMA.

Bwana Guterres kupitia ujumbe wake wa siku hii anasema pamoja na kutambua mchango wa wale walioko hai, kwa namna ya pekee wanatoa shukrani kwa walinda amani zaidi ya 3700 “waliolipa gharama ya uhai wao kwa kulinda wengine.”

 

 

“Na tunazienzi operesheni 14 zinazofanya kazi usiku na mchana kuwalinda watu na kuendeleza mchakato wa amani. Mwaka huu naitumia siku ya kimataifa ya walinda amani duniani nikiwa nchini Mali ili kuonyesha mshikamano wangu na wenzetu ambao wanakabiliwa na idadi kubwa ya majeruhi na hali tete.” Amesema Katibu Mkuu kupitia ujumbe wake.

Bwana Guterres amesema UN inapotambua umuhimu wa huduma na kujitolea kote duniani, pia inasimama kidete kuchukua hatua kwa ajili ya walinda amani- hatua za kufanya operesheni zetu kuwa salama na za ufanisi zaidi katika mazingira ya leo yenye changamoto.

Walinda amani wa UM wapiga doria Darfur Sudan. Picha: UNAMID
Walinda amani wa UM wapiga doria Darfur Sudan. Picha: UNAMID

Pia amesema wamejizatiti “kuimarisha jukumu muhimu ambalo vikosi vyetu vinastahili kulitekeleza katika kuchagiza haki za binadamu na kukabiliana na unyanyasaji na ukatili wa kingono.”

Katibu Mkuu amehitimisha ujumbe wake akisema kuwa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ni thibitisho la uwekezaji wa amani, usalama na ustawi duniani na kwamba, “kwa pamoja, hebu tuahidi kufanya kila tuwezalo ili kufanikisha mpango huo.”

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter