Watu zaidi ya 100 wauawa nchini Mali, Katibu Mkuu UN alaani vikali.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres
UN
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Watu zaidi ya 100 wauawa nchini Mali, Katibu Mkuu UN alaani vikali.

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo mjini New York Marekani, amesema amesitushwa na ripoti kuwa takribani watu 134 wakiwemo watoto na wanawake wameuawa na watu wengine takribani 55 kujeruhiwa kufuatia shambulio lililotekelezwa mapema leo jumamosi katika kijiji cha Ogossagou Peulh,Mopti katikati mwa Mali.

Bwana Guterres amelaani kitendo hicho na akatoa wito kwa mamlaka za Mali kuchunguza haraka na kuwafikisha katika mkono wa sheria waliohusika na shambulizi hilo la kutumia silaha.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatuma salamu zake za rambirambi kwa familia za waathirika, watu na serikali ya Mali na pia anawatakia kupona haraka wale wote waliojeruhiwa.

Katika kuisaidia serikali ya Mali, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA umetoa msaada kwa njia ya anga kuzuia mashambulizi zaidi na pia kusaidia kuwahamisha waliojeruhiwa.

Aidha Bwana Guterres ametoa wito kwa mamlaka nchini Mali kiuongeza maradufu jitihada zao za kurejesha amani na utulivu katikati mwa Mali.

Baraza la usalama nalo latoa tamko.

Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa awali limetoa tamko la kulaani vikali mashambulizi hayo ambayo yametekelezwa mapema leo jumamosi kwa kutumia silaha.

"Tunashutumu vikali mashambulizi haya ya kuhuzunisha," amesema François Delattre, Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa akizungumza kama Rais wa Baraza la Usalama katika mkutano wa waandishi wa habari Jumamosi jioni katika mji mkuu wa Mali, Bamako.

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mkuu wa MINUSMA wakizungumza na wanahabari katika mji mkuu wa Mali Bamako tarehe 23 Machi 2019.
MINUSMA/Harandane Dicko
Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mkuu wa MINUSMA wakizungumza na wanahabari katika mji mkuu wa Mali Bamako tarehe 23 Machi 2019.

 

Ujumbe wa Baraza umekuwa nchini Mali tangu mwishoni mwa wiki iliyopita kama sehemu ya ujumbe barani Afrika katika eneo lenye mzozo la Sahel. Ziara hiyo inatarajiwa kukamilika jumapili hii nchini Burkinafaso.

Mkoa wa Mopti ulioko katikati mwa Mali kwa muda umekuwa eneo la vurugu tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Jumapili iliyopita, kambi ya vikosi vya Mali FAMAs katika Kijiji cha Dioura ilishambuliwa na askari wake kadhaa wakapoteza maisha. Tarehe 26 mwezi Februari, watu 10 kutoka jamii ya Dogon waliuawa katika shambulizi lilotekelezwa kwenye Kijiji cha Gondogourou. Awali katika siku ya kwanza ya mwezi Januari, watu wasiofahamika wenye silaha waliwaua watu 37 katika Kijiji cha Kulogon cha jamii ya Fulani.