Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi zaidi zahitajika kupambana na magonjwa sugu -WHO

Usugu wa viuavijasumu kusababisha dawa kukosa kutibu. Picha: WHO

Juhudi zaidi zahitajika kupambana na magonjwa sugu -WHO

Afya

Hatua za haraka ni lazima zichukuliwe ili kukabiliana na magonjwa sugu pamoja na magonjwa  ya akili ambayo yanaongoza  kwa kusababisha vifo pamoja na changamoto za kiuchumi na kimaendeleo

Wito huo upo katika ripoti mpya iliyozinduliwa leo mjini Geneva Uswisi na tume  huru ya ngazi za juu kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza au NCDs ya shirika la afya ulimwenguni WHO.

Ripoti hiyo inasema magonjwa ya saratani, kisukari, matatizo ya kupumua na maradhi ya moyo  husababisha vifo vya watu milioni14 kwa mwaka ikiwa ni asilimia 71 ya  vifo vyote duniani. Idadi hiyo inajumuisha watu milioni 15 ambao hupoteza maisha mapema kati ya umri wa miaka 30 na 70 kutokana na NDCs.

Ripoti inamulika pia changamotoza matatizo ya akili na utipwatipwa ambazo mara nyingi hupuuzwa.

Akikabidhi ripoti hiyo kwa mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, rais wa Uruguay, Dkt Tabare Vazquez, amewataka viongozi duniani kuongeza mara dufu juhudi zao za kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa -NCDs angalau kwa theluthi moja ifikapo mwaka wa 2030 na bila kusahau afya ya kiakili.

"Kulinda na kuboresha hali ya maisha ya watu ni njia moja ya kuzidisha heshima ya mwanadamu ili kuweza kupiga hatua mbele za kiuchumi na kuishi pamoja," amesema Dkt Vazquez.Akaongeza,"..afya ni muhimu kwa amani na demokrasia kwani si suala la matumizi mengi bali malimbikizo bora."

Akipokea ripoti hiyo Dkt Tedros Ghebreyesus, amesema kuwa," WHO ilianzishwa mika 70 iliyopita kwa nia kuifanya afya kuwa ni haki ya kibinadamu na wala si faida kwa wachache." Ametoa wito kwa viongozi wa Dunia kuongeza mara mbili juhudi za kupambana na maradhi sugu ili kufikia lengo hilo.