Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kufanya mazoezi si lazima uwe mwanamichezo:WHO

Mazoezi ya yoga.(Picha:UM/Pasqual Gorriz)

Kufanya mazoezi si lazima uwe mwanamichezo:WHO

Afya

Huitaji kuwa mwanamichezo nyota kuufanyisha mazoezi mwili wako , kupanda ngazi badala ya kutumia lifti kunaleta tofauti kubwa. Kauli hiyo imetolewa leo na mkurugenzi mkuu wa shirika la afya ulimwenguni WHO, mjini Lisbon Ureno wakati wa uzinduzi wa mpango wa kimataifa wa kuwa na dunia yenye afya bora.

Kwa mujibu wa WHO kufanya mazoezi ni muhimu sana kwa afya, lakini katika dunia ya sasa inakuwa ni changamoto kubwa sababu miji na jamii hazijajengwa kwa mundo unaotakiwa kuwezesha azma hiyo.

Hata hivyo mkurugenzi huyo wa WHO Dr Tedross  Ghebreyesus amesema licha ya changamoto bado watu wanaweza kufanya mazoezi kwa mfano kutembea au kuendesha baiskeli badala ya kuendesha gari kwenda mwendo mfupi. Amesisitiza kuwa maamuzi tunayofanya kila siku ndio yatakayoweza kutuweka na afya njema ama la, akiwachagiza viongozi duniani kuhakikisha wanasaidia kufanya maamuzi hayo kuwa rahisi.

WHO inasema duniani kote mtu mzima mmoja kati ya watano na vijana barubari (wa miaka 11-17) wanne kati ya watano hawafanyi mazoezi ya kutosha, huku  wasichana, wanawake, wazee, watu masikini, watu wenye ulemavu na magonjwa sugu, watu waliotengwa na jamii za watu wa asili wakiwa na fursa finyu sana ya kuweza kufanya mazoezi.

Kwa mujibu wa mpango huo mpya “Tujishughulishe zaidi, kila mmoja kila siku” mazoezi ya mara kwa mara ni chachu ya kuzuia na kutibu magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) kama maradhi ya moyo, kiarusi, kisukari, na saratani ya matiti na utumbo.

Mpango huo unazionyesha nchi jinsi gani ya kupunguza hali ya kutofanya mazoezi kwa asilimia 15 ifikapo mwaka 2030, kwa kupendekeza sera 20 ambazo zinalenga kujenga jamii zenye afya kwa kuimarisha mazingira na fursa kwa watu wa rika zote hasa kuwafanya waweze kutembea zaidi, kuendesha baiskeli, na kushiriki michezo mbalimbali.