Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasafirishaji haramu wa binadamu wameua watu 12 Libya manusura wasaidiwa na UNHCR

Wakimbizi wakiwa katika meli ya Italy. Waliokolewa baada ya mashua yao kuzama nje ya mwambao wa Libya. Wenzao kama hao wanasaidiwa na UNHCR kurejeshwa nyumbani kwa hiari.
Picha ya UNHCR/Vania Turner
Wakimbizi wakiwa katika meli ya Italy. Waliokolewa baada ya mashua yao kuzama nje ya mwambao wa Libya. Wenzao kama hao wanasaidiwa na UNHCR kurejeshwa nyumbani kwa hiari.

Wasafirishaji haramu wa binadamu wameua watu 12 Libya manusura wasaidiwa na UNHCR

Haki za binadamu

Watu 12 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya wasafirishaji haramu wa binadamu nchini Libya kuwafyatulia risasi watu 200 waliokuwa wakishikilia mateka wakati walipojaribu kutoroka. 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR,  tukio hilo lilitokea Mei 23 kwenye mji wa Bani Walid uliopo Kusini Mashariki mwa mji mkuu Tripoli.

Watu hao 200 ni raia wa Eritrea, Ethiopia na Somalia na baadhi ya manusura wakielezea mkasa huo wamesema watu walipigwa risasi walipokuwa wakijaribu kutoroka lakini pia wasafirishaji haramu hao wa binadamu walipokuwa wakijaribu kuwakamata tena.

Hivi sasa manusura hao wanapatiwa msaada na UNHCR. William Spindler ni msemaji wa UNHCR Geneva anafafanua zaidi kuhusu tukio hilo

(SAUTI YA WILLIAM SPINDLER)

“Tunajua sasa kwamba watu wanashikiliwa na wasafirishaji haramu wa binadamu katika hali mbaya sana na mara nyingi wanauzwa katika utumwa mamboleo , kumekuwa na matukio mengi hadi sasa , visa vingi vilivyoorodheshwa vya watu kushikiliwa Libya katika mazingira mabaya sana na wasafirishaji haramu. Kisa hiki sio cha kawaida kwa sababu tunasikia watu walishikiliwa kwa kuwa walikuwa wanajaribu kutoroka katika maeneo hayo haramu.”

 Ameongeza kuwa manusura hao wengine wamekuwa mateka kwa takribani miaka mitatu. Uongozi wa Libya katika eneo hilo umewasafirisha watu 140 waliofanikiwa kutoroka na kuwapeleka kwenye kituo maalumu cha Gaser Ben Gashir Kusini mwa mji wa Tripoli.

Libya, wahamiaji, Wasafirishaji haramu wa binadamu, UNHCR