Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nuru na giza katika hatua za kuondoa nyuklia rasi ya Korea

Maktaba/UN
Taswira ya jaribio la nyuklia.

Nuru na giza katika hatua za kuondoa nyuklia rasi ya Korea

Amani na Usalama

Shaka na shuku rasi ya Korea baada ya mazungumzo yenye lengo la kusaka suluhu kusitishwa,  huku Korea Kaskazini ikitangaza kufunga eneo la majaribio ya silaha

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha  hatua ya Korea Kaskazini ya kufunga eneo lake la kufanyika majaribio ya nyuklia huko Punggye-ri.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Guterres pamoja na pongezi hizo ameelezea masikitiko  yake kwa kuwa wataalamu wa kimataifa hawakualikwa kushuhudia tukio hilo.

Hata hivyo amesema hatua hii mpya ya kutia matumaini itachangia juhudi zinazoendelea za kupata amani ya kudumu na kuondoa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea.

Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Guterres akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi amesikitishwa na taarifa za kusitishwa kwa mazungumzo kati ya Marekani na Korea Kaskazini.

Ninasikitishwa na taarifa za kufutwa kwa mkutano  uliopangwa kufanyika nchini wa Singapore kati ya  rais  wa Marekani na kiongozi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa  Korea. 

Mazungumzo hayo yaliyokuwa yafanyike tarehe 12 mwezi ujao huko Singapore yalilenga kusaka mbinu za kuondokana na silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea.

Tamko la Guterres linakuja kufuatia tangazo la kiongozi wa Marekani kupitia barua yake akieleza kuwa hatoshiriki tena katika mkutano huo.

Kiongozi huyo hakutoa sababu, lakini Bwana Guterres amezisihi pande zote kuendelea na mipango ya mazungumzo akisema,

(Sauti ya Antonio Guterres)

 “Nazihimiza pande zote  kuendelea na mazungumzo yao ili kupata njia  ya amani na inayofaa kuweza kuondolea rasi ya Korea silaha za Nyuklia.”