Wakimbizi wapya elfu 7 wa CAR wakimbilia kaskazini mwa DRC

18 Mei 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi UNHCR limeshtushwa na wimbi kubwa la wakimbizi wapya waliokimbilia kijiji cha Kazawi katika mkoa wa Bas- Uele, kaskazini mwa DR Congo wakitokea kusini mashariki mwa jamhuri ya Afrika ya kati CAR. 

 

Hiyo ni kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR William Spindler hii leo kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi ambapo amesema, zaidi ya wakimbizi wapya 7000 wameingia nchini humo ndani ya wiki moja iliyopita, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

(Sauti ya Wiliam Spindler)

“Wakimbizi wameripoti kukimbia mapigano mapya kati ya makundi mawili ya Anti-Balaka katika eneo la Kouango, mpakani. Na huu ni  mfululizo wa wakimbizi wanaokimbilia kaskazini mwa DRC ndani ya mwaka huu. Taarifa tulizo nazo ni kwamba idadi ya wakimbizi wa CAR nchini DRC imeongezeka kutoka 102,000 hadi 182,000, bila kuwajumlisha walioingia hivi karibuni.”

 Na kuhusu mikakati iliyowekwa na shirika hilo kuhusu upatikanaji wa huduma ya dharura kwa wazee, wanawake wajawazito na wengine ambao ni wahitaji wakubwa, Bwana Spindler amesema..

(Sauti ya Wiliam Spindler)

“Kuna chanzo kimoja tu cha maji katika kijiji cha Kanzawi, hivyo kuwalazimisha wakimbizi kunywa maji kutoka kwenye mto. Idadi kubwa ya  wakimbizi wanalala kwenye viwanja, wengine katika majengo ya umma.

Hata hivyo UNHCR imepongeza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kuacha mipaka yake wazi kwa ajili ya wakimbizi huku ikitoa wito wa usaidizi wa dharura ili kuunga mkono wenyeji wanaosaidia kuhifadhi wakimbizi hao.

Lengo ni kuhakikisha huduma kama vile maji, malazi na afya vinapatikana kwenye vijiji hivyo vilivyoko mpakani ambako idadi ya wakimbizi ni kubwa kuliko wenyeji.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud